NA MWAJUMA JUMA

WADAU wa Habari nchini wameiomba Serikali kuunda sheria rafiki ya vyombo vya habari itakayowawezesha waandishi wa habari kufanya kazi zao kwa uhuru.

Ombi hilo limetolewa na Ofisa Mipango Mwandamizi wa Baraza la Habari Tanzania (MCT) Shifaa Said Hassan, katika mkutano wa majadiliano kuhusu uhuru wa habari na vyombo vya habari uliofanyika njia ya mtandao.

Alisema wanatambua kwamba Serikali hivi sasa ipo katika mchakato wa kurekebisha sheria ya usajili wa wakala wa habari, magazeti na vitabu, hivyo ni matarajio yao kuwa italeta tija kwa vyombo hivyo.

Alisema masuala ya uchechemuzi katika habari yawe kwa pamoja na  waandishi wa habari wanatakiwa kulisimamia hilo kwa kuwa na sheria mpya na nzuri kwa waandishi wa habari.

“Suala la uhuru wa habari sio tu kuelekea kwenye demokrasia bali ni kwa waandishi wa habari wenyewe, tusimame kidete kulipigania hili, ili waandishi wafanye kazi zao kwa uweledi na uhuru”, alisema.

Ali Mbarouk kutoka Klabu  ya Waandishi wa Habari Pemba (PPC), akitoa mada kuhusu changamoto zinazowakumba waandishi wa habari alisema jambo la msingi kwa waandishi la kukamilisha malengo yake ni kujenga maslahi ya jamii na kubadilisha fikra na mitazamo hasi kupitia sauti zao.

“Sauti zetu zinatakiwa kuhakikisha zinaondosha mifarakano na kujaribu kutatua migogoro kwa jamii pamoja na kuwasaidia watu kufanya maamuzi sahihi na kuwa wawajibikaji”, alisisitiza Ali.

Aidha, alisema kutokana na kutokuwa na uhuru ndiko ambapo kunapelekea waandishi wa habari kuandika habari za matukio.

Rashid Omar mwandishi mwandamizi kisiwani hapa, alisema kuna haja ya kupatiwa mafunzo waandishi wa habari kuhusu sheria mpya, ili kuepuka kuja kukamatwa wakati wa kutekeleza majukumu yao.