Na Ali Shaaban Juma

IDADI ya wadudu warukao na wanaotambaa imekuwa ikipungua kwa kasi katika sehemu mbalimbali duniani kutokana na sababu kadhaa.

Kwa mujibu wa tafiti kadhaa zilizofanywa na taasisi mbalimbali ulimwenguni, idadi  ya wadudu imepungua kwa asilimia 50  ulimwenguni tokea mwaka 1970.

Katika hali ya kawaida watu wengi tunawaona wadudu kuwa ni kitu cha kawaida na kisicho na umuhimu mkubwa, lakini kwa uhalisia wa mzuko wa maisha, wadudu wana umuhimu mkubwa katika uhusiano wa maisha ya  watu na viumbe wengineo.

Mbali  ya kuwa wadudu ni chakula cha  binaadamu, popo, samaki na viumbe wengineo wanaotambaa kama vile mijusi, nyoka, vyura, bui, ndege na viumbe wengineo duniani, lakini pia wadudu huchangia kwa asilimia kubwa uhuwishaji wa udongo na maua na kuwezesha miti na mimea kutoa mazao ambayo ni chakula cha binaadamu, ndege na wanyama.

Kimaumbile, maua  ya miti  na mimea yana aina fulani ya unga ambao ili ua hilo liweze kutoa mbegu na hatimaye matunda ni lazima unga huo  wa maua usafirishwe kutoka  au  dume  hadi jike.

Kazi hiyo hufanywa na aina mbalimbali za wadudu ambapo baadhi  ya maua hutoa hafuru nzuri  wakati wa usiku  na kuwavutia baadhi ya viumbe kama vile popo ambao na husafirisha unga huo na kuhuwisha ua hilo na kutoa matunda.

Baadhi ya  miti na mimea huchanganya unga wa maua wenyewe na kuyawezesha maua hayo kutoa matunda. Lakini asilimia kubwa ya miti na mimea hutegemea wadudu, wanyama, upepo na maji kuhuwisha maua yake na kutoa mazao.

Kwa mtazamo wa haraka kupungua kwa wadudu duniani kuna maanisha kupungua kwa usambazaji wa mbegu za aina mbalimbali ya mimea  hali ambayo inahatarisha kupungua kwa mimea hiyo.

Minyoo inayoishi ardhini kama vile Nyungunyungu huchangia kwa kiasi kikubwa kurutubisha udongo na ni chakula cha viumbe wengineo. Nyungunyungu na minyoo mengineyo huishi kwa kula mabaki ya majani yaliyooza, ukungu unaoganda katika majani na mabaki mengineyo ya viumbe na vitu vya vilivyokufa, pia husaidia kuongeza hewa ya Oksijini katika mizizi ya miti na mimea na hivyo kurutubisha ardhi.

Mbali ya hayo, pia minyoo ni chakula cha baadhi ya wanyama wadogo wa porini kama vile Panya pori, Virodo, Kakakuona na wanyama wangineo. Udongo wenye rutba huwa na wastani wa minyoo 450 kwa mita moja ya mraba.

Si hayo tu, bali pia wadudu huchangia kusafisha mazingira kwa kuondosha baadhi ya uchafu unaoachwa na binaadamu na viumbe wengineo.

Asilimia 35 ya chakula kinacholimwa duniani kinategemea uhuwishaji wa maua unaofanywa na wadudu. Kazi inayofanywa na wadudu ya kusafirisha na kuchanganya unga wa maua na kuhuisha maua hayo na kuyawezesha kutoa mazao inakisiwa kugharimu  kati ya Dola za Marekani Bilioni 245 hadi Bilioni 577 kwa  mwaka duniani kote.

Kwa mujibu wa mtazamo wa kisayansi, kadiri idadi ya wadudu wanaohuwisha maua ya mimea wanavyopungua duniani kunapunguza idadi ya mazao yanayovunwa kutokana na kilimo ambapo pia kwa upande mwengine, idadi ya wadudu waharibifu wa mazingira wanaongezeka na kuchukua nafasi ya wadudu wanaohuwisha mimea na hivyo kuifanya dunia kuwa na idadi kubwa ya wadudu waharibu ambao kutaigharimu dunia mabilioni ya fedha hapo baadae.

Kwa mujibu wa utafiti ulofanywa na  shirika la “World Wildlife Fund” kwa kushirikiana na  “Zoological Society of London” na kuongozwa na Profesa Dave Goulson hapo mwaka 2018, imeelezwa katika ripoti ya utafiti huo iliyopewa jina, “Livingi Planet Report” kuwa idadi ya wadudu, samaki, wanyama, ndege na viumbe wanaotambaa wanaoishi majini na nchi kavu imepungua kwa asilimia 60  duniani katika kipindi cha miaka 34 kuanzia mwaka 1970-2014.

Kwa upande mwengine utafiti uliofanywa nchini Israel umeonesha kuwa idadi ya wadudu, samaki na viumbe wengineo wa porini imepungua duniani kwa asilimia 83% tokea kuanza kwa ustaarabu wa binaadamu ulimwenguni zaidi ya karne Ishirini zilizopita.

Utafiti mwengine ulofanywa mwaka 2019 katika maeneo 72  barani Ulaya na Marekani ya Kaskazini ikiwemo nchini Marekani, Canada na Mexico na Mwanasayansi aitwae Francisco Sanchez-Bayo

wa Australia umeonesha kuwa idadi ya wadudu katika maeneo hayo inapungua kwa asilimia  2.5% kila mwaka ambapo asilimia 41% ya wadudu wako katika hatari ya kumalizika.

Ripoti nyengine inayothibitisha kupungua kwa wadudu duniani ni ile iliyochapishwa mwaka 2017 nchini Ujerumani na kikundi cha Wanasayansi wa taasisi iitwayo “Krefeld Society” ambao kwa muda wa siku 17,000 katika kipindi cha miaka 26 kuanzia mwaka 1986-2014 walikuwa wakikusanya kwa mitego maalum wadudu warukao katika maeneo 63 ya hifadhi za taifa nchini humo na kupata wadudu wenye uzito wa Kilo 53.

Ripoti  ya utafiti huo umeonesha kuwa idadi ya wadudu warukao nchini Ujerumani imepungua kwa asilimia 75% katika kipindi hicho cha miaka 26.

Nyuki ambao ni wadudu muhimu sana ulimwenguni kutokana na kutengeneza asali na kuchangia kwa kiasi kikubwa katika kuhuwisha maua ya miti na mimea, wamekuwa wakipungua kwa kasi mno duniani.   Kwa mujibu wa ripoti ya utafiti ulofanywa na Jumuiya ya Ulaya hapo mwaka 2018, asilimia 9.2 ya nyuki barani humo wako hatarini kumalizika.   Kwa ujumla kati ya aina  kadhaa za nyuki wanaojulikana kuwepo barani Ulaya, aina 150 za nyuki ambao ni sawa na asilimia 7.7 wamepungua kwa kiwango kikubwa.

Uzalishaji wa asali umepungua duniani kwa asilimia 30 katika miaka kumi iliyopita kutokana na kupungua kwa nyuki duniani.

Mbali ya nyuki, takwimu hizo za barani Ulaya zinaonesha kuwa asilimia 16% ya Tandarusi, asilimia 9 ya vipepeo, asilimia 23 ya viumbe wanaoishi  majini na nchi kavu, asilimia 20 ya jamii ya mijusi na asilimia 40 ya Minyoo na Konokono wa  maji baridi wamepungua barani humo.

Ingawa hakuna taarifa sahihi za tafiti kuhusiana na kupungua kwa baadhi ya wadudu maarufu duniani kama vile Panzi, Mzigu mzigu, Nzi, Vunja jungu na wengineo, lakini wanasayansi wamekuwa wakitumia kigezo cha kupungua kwa idadi ya ndege warukao wanaokula wadudu kuthibitisha kupungua aina hizo za wadudu ambao ni chakula cha ndege hao.

Idadi ya ndege wanaokula wadudu inapungua kwa kasi katika maeneo mbalimbali ambapo kati ya mwaka 1966-2013 idadi ya ndege wanaokula wadudu imepungua kwa asilimia 43 huko Marekani ya Kaskazini.

Huko nchini Uingereza idadi ya Msese imepungua kwa asilimia 93 kati ya mwaka 1967-2013. Ndege wengine waliopungua  kwa asilimia kubwa kutokana na kupungua kwa wadudu nchini Uingereza ni pamoja na wale waitwao “Grey partridge” waliopungua kwa asilimia 92, “Nightingale” waliopungua kwa asilimia 93 na “Cuckoo”  waliopungua kwa  asilimia 77 , Pia ndege waitwao “Red-backed shrike” wanaokula wadudu wakubwa wamemalizika nchini Uingereza katika miaka ya 90.

Pamoja na mambo mengine kupungua kwa idadi ya wadudu ulimwenguni hasa katika mataifa yaliyoendelea kiviwanda kumetokana na sababu kadhaa. Sababu hizo ni pamoja na uchafu wa mazingira  kunakosababishwa na hewa chafu ya viwandani, ukataji wa misitu, kupungua kwa giza ulimwenguni pamoja na wadudu hao kupoteza maeneo ya kuishi kutokana na ujenzi wa miji, utanuzi wa mashamba na ujenzi wa miundombinu mengineyo.

Si hayo tu, bali pia kupungua kwa wadudu ulimwenguni kunatokana na matumizi ya madawa ya kunyunyiza  ya kuua wadudu waharibifu mashambani.

Sababu nyengine inayochangia kupungua kwa wadudu duniani ni mabadiliko ya tabia nchi pamoja na wadudu hao kufa kutokana na maradhi yanayoenezwa na wadudu wengineo wasio wa asili wanaoingizwa katika mataifa mengineyo.

Hakuna taarifa sahihi za idadi au kiwango cha wadudu waliomalizika katika msitu Mkuu wa Amazon huko Marekani ya Kusini, Msitu wa Congo barani Afrika na Misitu mikubwa ya Indonesia na sehemu nyenginezo barani Asia, lakini utafiti ulofanywa kwa miaka 35 kati ya mwaka 1976- 2013 katika msitu mkuu wa Puerto Rico na mwanasayansi wa Marekani  aitwae Bradford C. Lister  umeonesha kuwa Mabui na wadudu wengineo wamepungua  kwa asilimia 75- 98 katika kipindi hicho.