NA LAYLAT KHALFAN

MAMLAKA ya Usafiri na Usalama barabarani Zanzibar, imesema itaendelea kutoa miongozo ya kibiashara kwa waendesha boda boda baada ya kurasimishwa rasmi kazi hiyo.

Ofisa kutoka Mamlaka hiyo, Hassan Vuai Mchanda, aliyasema hayo wakati akizungumza na waendesha bodaboda hizo kwa Wilaya ya Magharibi ‘A’ Unguja.

Alisema miongoni mwa miongozo hiyo ni pamoja na ukataji wa leseni kwa wanaoendesha vyombo kama hivyo ikiwemo bodaboda na bajaji na nyengine ambazo zitakuwa na mnasaba wa kufanya shughuli hiyo.

Aidha, Mchanda alifahamisha kuwa, kwa vile kazi hizo wanazozifanya wafanyabiashara hao zina changamoto nyingi kwao na baadhi yao ni kero kwa wananchi, hivyo kufanya hivyo kutawarahisishia utendaji kazi zao na kuwaondolea matatizo yaliyokuwa yakijitokeza muda mrefu.

“Kwa vile biashara hii itakuwepo kisheria na kufuata miongozo na kanuni zinazoelekeza za mamlaka hii mutaweza kufanyakazi zenu kiurahisi na kujiingizia kipato kutokana na kufanya usajili huo”, alisema.

Akifungua mkutano wa waendesha bodaboda, Mkuu wa Wilaya ya Magharibi ‘A’ Suzan Peter Kunambi, alisema ipo haja kwa waendesha vyombo hivyo kufuata taratibu na sheria zilizowekwa bila ya kupinzana na sheria iliyopo  kwani itawajengea mustakbali mzuri wa kazi zao za kila siku.

“Kilichobaki kwenu ni kufuata masharti tu, ili mtambulike kisheria msifanye ajizi juu ya suala hili wenyewe mtakuwa mnajitafutia matatizo yasiyokuwa na ulazima”, alisema Kunambi.

Alisema wengi wao wanaoendesha biashara hiyo hawana leseni, hivyo aliwataka kutumia fursa hiyo kwa lengo la kuwasaidia na kuwajengea uaminifu kwa abiria wao wanaowachukua.

Alisema endao watafanya hivyo jamii itawaamini sambamba na kuondosha matatizo ikiwemo kufanya vitendo viovu ambavyo vimekuwa vikiathiri jamii siku hadi siku.

Nao wafanyabashara wa boda boda waliiomba Mamlaka hiyo kuwaondoshea baadhi ya kero mbali mbali zinazowakabili ikiwemo kuwarahisishia upatikanaji wa leseni ili waweze kufanya biashara zao kwa ufanisi zaidi.

“Tushakubali kufuata masharti na miongozo yaliyomo kwenye shughuli hizi, kwa kuwa ndio tegemeo letu kubwa la kujipatia kipato, hivyo huduma tupatiwe haraka ili tuendelee na majukumu yetu”, walisema.