NA KASSIM ABDI, OMPR

MAKAMU wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Hemed Suleiman Abdulla amewataka wafanyabiashara nchini kuacha tabia ya upandishaji wa bei za bidhaa kiholela ili kuwapunguzia wananchi ukali wa maisha.

Makamu huyo alieleza hayo katika kikao maalum kilichowakutanisha viongozi wa wizara, wafanyabishara na maofisa wa usimamizi wa kodi kwa lengo la kulipatia ufumbuzi tatizo la upandaji wa bei za bidhaa.

Hemed alisema si jambo linalopendeza kwa wafanyabiashara kukiuka miongozo na taratibu zilizowekwa na serikali juu ya bei za bidhaa kutokana na upandishaji wa bei unasababisha usumbufu kwa wananchi hasa wale wa kipato cha chini.

Alieleza kuwa wananchi wamekuwa wakiitupia lawama serikali kwa kuona hakuna unafuu wa bidhaa hasa za chakula jambo linalosababishwa na wafanyabiashara wasiokuwa waaminifu.

Katika kikao hicho Makamu wa Pili wa Rais alilazimika kupiga simu kwa wauzaji wa bidhaa kutoka nje ya nchi ili kulinganisha gharama za bei wanazonunulia wafanyabiashara hao na bei wanazowauzia wananchi na kugundua kuwa kuna utofauti mkubwa kati ya bei hizo.

Aliwataka wafanyabiashara hao kupunguza bei za bidhaa mara moja kabla serikali haijachukua hatua za kinidhamu dhidi ya wafanyabiashara wasiokuwa waaminifu kwa kuwafutia kibali cha kufanya biashara Zanzibar.

Akichangia katika kikao hicho waziri wa Biashara na Maendeleo ya Viwanda Omar Said Shaaban alisema kuwa wafanyabiashara wana tabia ya kukacha kutoifuata miongozo inayowekwa na serikali katika uuzaji wa bei za bidhaa.

Kwa upande wake waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Fedha na Mipango, Jamal Kassim Ali alisema kuwa wananchi wa Zanzibar hawana jukumu la kuwachangia mitaji wafabyabiashara katika kuendesha biasgara zao, hivyo suala la kupandisha bei za bidhaa bila ya kufuata taratibu halikubaliki.

Nae, mfanyabisha maarufu Zanzibar, Said Bopar aliwataka wafanyabishara wenziwe kuwa waaminifu kwa kuwaonea huruma wananchi kutokana na upatikanaji wa bidhaa hizo katika soko kuwa wa kuridhisha.

Katika kikao hicho kilichowakutanisha wadau kutoka sekta mbali mbali kimetoka na azimio kwa bei ya dumu moja la mafuta liuzwe shillingi 75,000 kutoka shilingi 80,000.