NOUAKCHOTT, MAURITANIA

WAHAMIAJI wapatao 47 wamepatikana wakiwa wamefariki hapo juzi huko pwani ya Nouadhibou, kaskazini magharibi mwa Mauritania, Shirika la Kimataifa la Uhamiaji (IOM) na Shirika la Wakimbizi la Umoja wa Mataifa (UNHCR) yalisema.

Kulingana na taarifa iliyopokelewa na Xinhua, mashua iliyokuwa imewabeba wahamiaji hao iliondoka Agosti 3 kutoka pwani ya Atlantiki ya Afrika Kaskazini kuelekea Visiwa vya Canary na ilikuwa imebeba watu 54, wakiwemo watoto watatu.

“Baada ya siku mbili baharini, kutofanya kazi kwa injini kuliwaacha abiria wakiwa wamekwama bila chakula au maji kwa karibu wiki mbili. Walipoonekana na walinzi wa pwani ya Mauritania mnamo Agosti 16, ni watu saba tu walikuwa bado hai, wanne kati yao wakiwa katika hali mbaya , “ilisema taarifa hiyo.

Msiba huo ulitokea siku 10 baada ya vifo cha wahamiaji wengine 40 kwenye njia hiyo hiyo, mashirika hayo mawili yaliongeza. Kulingana na IOM, mnamo Januari 2021, zaidi ya watu 350 walikufa, wakati zaidi ya wakimbizi 8,000 na wahamiaji walifika Uhispania kupitia njia hio ya baharini.

Tangu Oktoba 2020, zaidi ya watu 1,200 wameokolewa kutoka pwani ya Mauritania na kupokea msaada wa matibabu kama sehemu ya mpango wa huduma ya kwanza iliyowekwa na IOM.

IOM na UNHCR wanaomba msaada zaidi ili kuweza kuendelea na hatua zao za kuokoa maisha, pamoja na uchunguzi na msaada wa matibabu na wa kisaikolojia.