PORT-AU-PRINCE, HAITI
MSAADA umeanza kuwasili kwa wingi kwa wahanga wa janga la tetemeko la ardhi na kimbunga vilivyoikumba Haiti lakini hali duni ya miundombinu nchini humo inatatiza zoezi la kuwafikia walioathirika.
Misaada kutoka kwa taasisi binafsi na shehena nyengine iliyotumwa na Marekani na mataifa mengine imeanza kulifikia eneo la kusini magharibi mwa Haiti ambako tetemeko kubwa la ardhi la Jumamosi iliyopita limewauwa zaidi ya watu 2,100.
Taarifa zinasema juhudi za kusambaza mahitaji zinakwenda pole pole kutokana na athari ya mvua kubwa iliyosababishwa na kimbunga kilichopewa jina Grace kulichokipiga kisiwa hicho cha Karrebian.
Hadi sasa shirika la Usalama wa Umma nchini Haiti limesema idadi ya waliokufa kutokana na tetemeko la ardhi imepanda na kufikia watu 2,189 na wengine 12,268 wamejeruhiwa.