KIJIOGRAFIA Zanzibar ni visiwa vilivyozunguukwa na bahari, ambapo pamoja na visiwa viwili vikubwa vya Unguja na Pemba, pia ina visiwa vidogo kadhaa, ambapo baadhi yao vinakaliwa na watu na visivyokaliwa na watu.
Ardhi ya Zanzibar kwa ujumla inaelezwa kuwa haizidi kilomita za mrada 1,666, jambo baya zaidi ardhi hii haiongezeki huku idadi ya watu ikiongezeka kila uchao.
Udogo huo huo wa ardhi tuliojaliwa kuwa nao kama Zanzibar, tunapaswa tuutumie vizuri kwa ajili ya makaazi, kilimo pamoja na harakati nyengine zitakazoweza kuendeleza maisha yetu.
Awamu ya kwanza ya serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, chini ya hayati mzee Karume, katika kuhakikisha wananchi wanajitegemea, alitekeleza sera ya wananchi kugaiwa eka tatu ili aweze kuzalisha chakula na mazao ya biashara.
Mantiki hasa ya mzee Karume kugawa eka tatu, chanzo chake kilitokana na chini ya utawala wa kisultani uliodumu kwa miaka kadhaa, wananchi wazalendo wa Zanzibar hawakuweza kumiliki ardhi hali iliyowafanya kuwa masikini sana.
Kwa wakati huo wengi wao walikuwa wakifanyakazi kama manamba kwenye mashamba ya chakula na mazao ya biashara yaliyokuwa yakimilikiwa na mabwanyeye waliokuwa na fursa kubwa kwenye utawala wa kisultani.
Baada ya Mapinduzi matukufu ya mwaka 1964, mzee Karume ndipo akaanza kuitekeleza sera ya kuwagaia wananchi eka tatu, hata hivyo kinyume na malengo ya mzee Karume hivi sasa mambo yamekuwa hayendi vizuri kwa waliopewa ekari hizo.
Kwa bahati mbaya sana wapo waliodhani kwamba ekari hizi wamegaiwa kwa maana kwamba ni milki yao, jambo ambalo sio sahihi, ukweli ni kwamba ekari hizo waliazimwa si gaiwa kwani ardhi yote mali ya serikali.
Kutokana na kudhani kwamba wamegaiwa na ziko kwenye miliki zao, inasikitisha sana kuona baadhi ya waliopewa mashamba ya ekari hizo wameyafisidi kiasi kwamba hata yangekuwa mali yao wasingeweza kufanya hivyo.
Bila shaka hujuma walizozifanya zinatokana na kwamba ardhi hizo walizopewa na serikali haziwaumi, hawana uchungu zao na wala hawajali, ndio maana wamediriki hata kukata viwanja na kuviuza kwa ajili ya nyumba za makaazi.