NA SABRA MAKAME,SCCM
MKAGUZI wa Dawa na Vipodozi, Abdulfatah Nassor Issa, amewahimiza wajasiriamali wadogo kuhakikisha bidhaa wanazotengeneza zinasajiliwa ili kuhakikisha usalama kwa watumiaji.
Aliyasema hayo akiwa ofisini kwake Mombasa wakati akizungumza na Zanzibar Leo baada ya kupata taarifa kuna wajasiriamali wanauza bidhaa ikiwemo kirimu bila ya kufuata utaratibu uliowekwa.
“Maabara ya Wakala wa Chakula, Vipodozi na Dawa, huchunguza ubora na Usalama wa bidhaa zote zinazodhibitiwa na (ZFDA) ikiwemo dawa za miti shamba, dawa asili na vipodozi kabla ya kuepo sokoni, ili kuepusha madhara kwa watumiaji” alisema Abdulfatah.
Alisema kifungu namba 16 na 18 cha sheria ya chakula, dawa na vipodozi kinakataza kuuza, kuhifadhi au kusindika chakula kwenye jengo ambalo halijasajiliwa na wakala.
Alisema wamekua wakitoa elimu kwa vyombo mbali mbali vya habari kuhakikisha wajasiriamali wote wanakamilisha utaratibu kuanzia pale ambapo bidhaa inatengenezwa mpaka itakapofikia sokoni.
Aidha, alisema kesi nyingi zinazowaathiri watumiaji wa vipodozi zinatokana na matumizi mabaya ya bidhaa ambazo hazijasajiliwa.
“Katika kuhakikisha watu wanajisajili lazima bidhaa inayouzwa ipite maabara kutizama kiwango cha chemikali ambayo imo kwenye ‘cream’ ikiwa imezidi tunamuelekeza kupunguza, ili kuondosha madhara”alisema Mkaguzi.
Alisema kwa yeyote ambae anafanya biashara bila ya kuzingatia ubora wa bidhaa hiyo kuwa na athari kwa watumiaji atachukuliwa hatua baada ya kuthibitishwa kuwa ni mkosa.
Mkaguzi alieleza ni muhimu kwa wajasiriamali kuhakikisha wanaeka stika nje, ili iweze kumtambulisha mmiliki wa bidhaa na atakapohitajika kuepusha usumbufu.
Vile vile alisema kwa yeyote ambae anaeuza bidhaa kama sabuni, vipodozi vya aina yeyote hususani vya kutengeneza wenyewe bila ya kujisajili au vilivyomletea madhara mtu asiache kutoa taarifa ofisini kwao Mombasa.
Abdulfatah aliwashauri wananchi kujisajili mapema vile vile kuhakikisha vipodozi wananunua katika dawa kwani ni sehemu ambazo huthibitisha bidhaa zenye uhakika na salama kwa afya zao.