KWA zaidi ya miaka 200, Zanzibar nchi mashuhuri duniani kutokana na uzalishaji wa zao la karafuu kiasi kwamba pale unapotaja jina la visiwa hivi jambo la kwanza kwenye fikra za walimwengu ni karafuu.
Sio kama huko duniani hakuna nchi nyengine zinazozalisha karafuu, zipo nchi tele tena zinazalisha kwa wingi karafuu pengine hata kuliko Zanzibar, lakini ukweli ni kwamba karafuu za Zanzibar ni za kipekee.
Upekee huo ndio unaoling’arisha jina la Zanzibar duniani kote tangu muda hadi hii leo na kwamba pale karafuu za visiwa hivi zinapoingia kwenye soko la ulimwengu wengine akina Brazil, Indonesia husubiri kwanza tuuze sisi.
Hata hivyo, uzalishaji wa zao la karafuu visiwani hapa, umepita kwenye misukosuko mingi kwenye vipindi tofauti ikiwemo kuanguka thamani kwenye soko la dunia.
Aidha changamoto nyengine ililolikumba zao hilo, katika miaka ya karibuni kabisa, ni suala la baadhi ya wafanyabishara kuzinunua kinyemela kwa wakulima na kuzisafirisha kwenda nchi jirani.
Ingawaje tatizo la magendo limepungua sana, lakini wakulima wa karafuu walipigwa kasumba ya kutosha na wafanyabishara hao wanaozitorosha nje ya nchi karafuu wakisingizia serikali kupitia Shirika la Biashara la Taifa (ZSTC), inazinunua kwa bei ndogo.
Serikali ilikata pua na kuunga wajihi kwa kufanya uamuzi wa makusudi kulipandisha bei zao hilo, ambapo bei inayonunua kwa kilo inalingana sana na ile ya soko la dunia.
Ukiangalia ama ukitafakari bei ya zao la karafuu kwa wakati huu haihitaji akili ya shahada, uzamili ama uzamivu, kugundua kuwa bei ya sasa iliyopangwa na serikali ni muafaka sana na ukweli ni kwamba kuzisafirisha nje ni kujisumbua na kutafuta hasara.
Kwa wale wazito wa kufahamu, hasara ya kwanza huko zinakopelekwa bei ni ndogo ikilinganishwa na bei zinazonunuliwa na serikali, lakini pia sheria inaweka wazi pale zinapokamatwa kimagendo hutaifishwa karafuu zenyewe na chombo kinacho safirishia.
Tungependa sana kuwasihi wakulima na wafanyabishara wa karafuu kwa wakati huu zao hilo likuwa kwenye mavuno kutojihuisha na mgendo, kwani kufanya vitendo hivyo ni kusababisha hujuma dhidi ya uchumi wa nchi.
Kwa mfano serikali inanunua karafuu na kuziuza nje ya nchi, baada ya kupata fedha za kigeni ndiyo hizo zinazotumika kuifadhili miradi ya kijamii ambayo inatumiwa na wananchi wote.
Bila shaka na ni ukweli ulio wazi, wanaofanya magendo wamekosa uzalendo wa kuijenga nchi yao, kibaya zaidi ndio hao wanaolaumu serikali hijafanya hili, serikali hijafanya lile.
Tunadhani kabla ya lawama za kwamba serikali hijafanya hili na lile, kwanza ungejilaumu wewe kwa kujiuliza masuali ya uzalendo ameifanyia nini nchi yako? je huna lolote la kuifanyia nchi yao?
Tuungane na kauli ya serikali ya kuwataka wakaulima wote wauze karafuu zao katika maduka ya Shirika la Biashara la Taifa la Zanzibar (ZSTC), ambapo shirika hilo linanunua karafuu kwa mujibu wa bei ya soko la dunia.
Aidha kabla ya kuhusisha vikosi vya ulinzi wananchi wenyewe wawe tayari kuhakikisha wanawafichua wale wachache wenye tabia ya kufanya magendo ya karafuu.
Tunajua wasafirisha magendo ya karafuu nje ya nchi wana mbinu nyingi, lakini tunaamini mbinu zao zote serikali inazifahamu na imejipanga kuhakikisha inakabiliana na wale wote wenye tabia hiyo.