NA YUSSUF ALI (WAMM)

WAZIRI wa Ardhi na Maendeleo ya Makaazi, Riziki Pembe Juma, amewataka walimu kufanyakazi kwa uadilifu, bidii, uaminifu na mashirikiano, ili kuweza kukuza sekta ya elimu nchini.

Waziri Pembe, aliyasema hayo huko skuli ya Mwembemakumbi, wakati alipokuwa akizungumza na walimu pamoja na  wanafunzi katika mahafali kumuaga aliekuwa mwalimu wa skuli hiyo, Mtukwao Khatib Hamadi.

Mwalimu huyo amemaliza muda wake wa kiutumishi Serikalini katika sekta ya elimu na kuambatana na utoaji wa zawadi kwa wanafunzi 14 ambao wamefaulu katika vipawa maalum kuendelea na masomo yao katika skuli mbali mbali.

Alisema kuwa mashirikiano baina ya mwalimu na mwanafunzi ndio njia pekee itakayomuezesha mwanafunzi kufaulu katika mitihani yake..

Kutokana na hali hiyo Waziri huyo alisema walimu hawana budi kufanyakazi kwa bidii zaidi na maarifa pamoja na ustahmilivu wakifahamu kuwa kazi ya elimu ni wito.

Alieleza kuwa ni fahari kubwa kuona skuli hiyo inatoa wanafunzi wenye vipawa maalum, hivyo alisisitiza haja ya kuendeleza kuwa na uzalendo na mapenzi makubwa kwa wanafunzi kwani matunda yao ni fahari kubwa kwa walimu.