SERIKALI ya Mapinduzi ya Zanzibar ilichukua mkopo Benki ya Dunia unaofikia takriban dola 93,000, kwa lengo la kutekeleza miradi ya kung’arisha na kupendezesha miji.
Miongoni mwa miradi hiyo ambayo ilitekelezwa chini ya mradi wa Huduma za Jamii Mijini (ZUSP) ni pamoja na ujenzi wa mitaro ya kuondosha maji katika maeneo yenye kutuwama hasa wakati wa mvua za masika ambapo ilikuwa kawaida kutokea mafuriko.
Maradi mwengine muhimu uliotekelezwa chini ya ZUSP ni uwekaji wa kamera za usalama (CCTV), katika maeneo kadhaa. Kamera hizo zinasaidia sana kuwafichua wale wanaojihusisha na vitendo vya uhalifu katika barabara zetu.
Kama tunavyoelewa miji haiwezi kung’ara pasi na barabara kuwa na taa, ambapo chini mradi wa ZUSP, barabara mbalimbali za miji ya Unguja na Pemba zimewekwa taa za kisasa.
Kiukweli barabara zilizoekwa taa utapenda kuzitemebelea wakati wa usiku pasi na kuwa na hofu yoyote ya uhalifu, kwani mtu aliye umbali wa zaidi ya mita 200 unaweza kumuona bila ya shaka yoyote.
Taa hizo pia zimewekwa makusudi kwa ajili ya kupunguza ajali za barabarani hasa zile zinaotokea wakati wa usiku.
Tukumbuke kuwa kabla ya kuekwa kwa taa hiso, Jeshi la Polisi mara kwa mara lilikuwa likitoa taarifa kwamba barabara kutokuwa na taa wakati wa usiku kunasababisha ajali.
Wakati ikiwa hata mwaka mmoja haujatimia tangu taa hizo kuekwa, katika baadhi ya barabara haziwaki, tukitolea mfano sehemu kubwa ya barabara ya Mkapa.
Ulipofanywa uchunguzi kilichobaikina kumbe kuna vijana tunaoweza kuwaita kuwa ni wahujumu wanazifungua taa hizo na kuiba nyaya za shaba na kwenda kuziuza katika maduka yanayonunua mali chakavu.
Kwanza tuzipongeze hatua za jeshi la polisi kwa kutekeleza wajibu wake hasa pale walipofanikiwa wakutia mbaroni baadhi ya vijana wanaojishughulisha wizi wa nyanya hizo.
Kiukweli huhuma zilizofanywa na wahalifu hao ambapo isikitisha kusikia baadhi yao ni wanafunzi wa skuli za sekondari, zimesababisha hasara kubwa kwani jumla ya nyaya zenye urefu wa zaidi ya mita 11,150 zimeibiwa.
Taarifa zaidi zinaeleza kwamba zaidi ya nguzo 175 za taa za barabarani zimekumbwa na hujuma za kuibiwa nyaya ambapo wilaya ya Magharibi ‘A’, nguzo 55 zenye waya wa mita 2,750 na nguzo 120 zenye waya wenye urefu wa mita 4,200 katika wilaya ya Mjini.
Kwa mujibu wa taarifa wahujumu hao wanauza nyaya hizo katika maduka mahususi yenye kununua bidhaa chakavu ikiwemo kampuni ya Zanzibar Steel Co. Ltd ililopo Kwamchina, wilaya ya Magharibi ‘B’ ambayo imenunua kilo 4,613 kutoka kwa wagalifu hao.