ALGIERS, ALGERIA
IDADI ya watu waliopoteza maisha baada ya moto mkubwa kuteketeza misitu katika mkoa wa Tizi Ouzou nchini Algeria imefikia 42.
Ayman bin Abdul-Rahman, Waziri Mkuu wa Algeria alisema kuwa, moto huo ulioanza siku ya Jumatatu hadi sasa umesababisha vifo vya raia 17 na wanajeshi 25.
Rais Abdelmajidjid Tebboune wa Algeria ameandika katika ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa twitter kwamba, wanajeshi 25 walifariki wakati walipokuwa katika juhudi za kuwaokoa raia waliokuwa wamekwama katika moto.
Mamlaka ya Ulinzi wa Rais ilisema katika taarifa yake kwamba, akthari ya nyumba zilizokuwa zinapakana na misitu inayoteketea moto katika mkoa huo wa Tizi Ouzouu ulioko yapata kilomita 150 mashariki mwa mji mkuu Algiers, zimebakia majivu kutokana na moto huo.
Gazeti la al-Bilad la nchi hiyo limeripoti kuwa, skuli za mkoa wa Tizi Ouzou zinawapokea wananchi waliolazimika kuwa wakimbizi wa ndani kutokana na mkasa huo wa moto wa misituni.
Habari zaidi zinasema kuwa, zaidi ya visa 70 vya misitu kuteketea kwa moto vimeripotiwa katika mikoa 18 ya kaskazini mwa nchi hiyo ya kaskazini mwa Afrika katika siku za hivi karibuni.
Wakati baadhi ya viongozi wa Algeria wakisema kuwa, chanzo cha moto huo ni kupanda kwa kiwango cha joto, ushahidi unaonyesha kuwa, chanzo cha moto huo ni sababu za kibinadamu.