NA SABRA MAKAME, (SCCM)

MKURUGENZI Mipango Sera na Utafiti Ofisi ya Rais Fedha na Mpango, Saumu Khatib Haji amewatoa hofu wananchi ambao wamejiunga na kampuni ya Master Life Microfinance Limited kuhakikiwa ili wapatiwe haki inayostahili.

Aliyasme hayo Ziwani Polisi wakati akiwa katika muendelezo wa uhakiki kwa wananchi ambao wameweka fedha zao katika kampuni ya Master life.

“Tunafanya uhakiki huu ili tuwatambue nani na nani suala hilo lililomgusa kama ambavyo mahakama imetuamrisha, leo ni siku ya nne tangu zoezi hili limeanza”alisema saumu

Alisema zoezi la uhakiki kwa sasa linaendelea katika wakaazi wa Mkoa wa Mjini Magharibi Wilaya ya Magharibi ‘B’  ambalo zoezi hilo litadumu kwa muda wa siku mbili.

Mkurugenzi alisema kwa wale ambao wakaazi wa Magharibi ‘A’ zoezi hilo litaanza leo na Jumapili ya mwezi huu katika skuli ya Bububu jengo jipya.

Aidha, Mkurugenzi amewataka wananchi kuacha tabia ya kujitokeza katika vituo ambavyo hawajapangiwa, ili kuepusha usumbufu.

Nae Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya kuzuia Rushwa na Uhujumu Uchumi (ZAECA), na ni Mwenyekiti wa Kamati ya uhakiki Master Life, Khamis Ahmed Makarani, alisema wapo katika muendelezo wa kuhakiki wananchi, alisema hali mpaka sasa ni salama wananchi wasiache kujitokeza.

“Watu wengi wamejitokeza  kuhakiki majina yao na wasivunjike moyo waendelee na zoezi hilo kwa kufuatilia ratiba ambazo zinatolewa na wahusika”alisema