NA SABRA MAKAME (SCCM)
KAIMU Mwalimu Mkuu wa skuli ya Kwa Mtipura, Ghanima Ali Abdalla amewataka wanafunzi wa skuli hiyo wanaojishirikisha kufanya uhalifu waache kufanya hivyo kwani serikali imekuwa ikitumia fedha nyingi kwa ajili ya kuweka mazingira bora ya skuli.
Akizungumza na Zanzibar Leo ofisini kwake Kilimahewa Mkoa wa Mjini Magharibi, Ghanima amesikitishwa na uhalifu unaofanywa na baadhi ya wanafunzi wakishirikiana na wananchi katika skuli hiyo kwa kulingo’a geti la skuli na kulipeleka kusipojulikana bila ya kugundua nani aliyeshiriki tukio hilo.
Aidha alisema tukio hilo lilitokea majira ya saa 9:00 mchana wakati walimu wakiwa madarasani wanafundisha na baada ya kutoka nje hapakua na mtu na geti ambalo lipo mlangoni kwa ajili ya kuingia na kutoka walilikuta halipo na ndipo taarifa zilipoanza kuenea.
Alieleza kuwa awali hawakujua nani ambae anatuhumiwa kosa ilo ,miongoni mwa mfanya biashara wa skuli hiyo alitoa taarifa kwa mkuu huyo baada ya kushuhudia geti likitolewa na wanafunzi wawili waliovaa sare ya skuli.
Pia Mfanyabiashara huyo alisema baada ya kung’olewa geti hilo vijana wawili wa kiume walishirikiana na wanafunzi kuondoka nalo maeneo mengine ambayo mbali na skuli hiyo.
Ghanima alisema tayari taarifa hiyo ameshaifikisha kwa sheha wa Kilimahewa na Kwamtipura kutokana na wote wanajumuika katilka skuli hiyo, ambapo waliwatuma vijana kuwasaka watu hao kwani wafanyaji ni wakaazi wa mitaa ya skuli.
Hata hivyo alisema wameanza kutafuta mbadala wa tatizo hilo, ili kuimarisha usalama wa skuli hiyo, na bado wanaendelea na uchunguzi wa kuweza kubaini nani ambae amefanya tukio hilo ,na sheha amekabidhiwa majina ya wahusika wote akifuatilia kiundani zaidi.