NA HAFSA GOLO
SERIKALI ya Mapinduzi Zanzibar imeshauriwa kuchukua maamuzi mapema ya kuwaondosha wananchi wanaoishi katika maeneo hatarishi kwenye msitu wa Masingini, ili kulinda usalama wao na kudhibiti athari nyengine zinazoweza kutokea .
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Mazingira Sheha Mjaja Juma, alitoa ushauri huo alipokua akizungumza na gazeti hili ofisini kwake Maruhubi.
Alisema iwapo serikali haitochukua tahadhari mapema ya kuwahamisha wakaazi wa maeneo hayo upo uwezekano mkubwa wa kujitokeza athari mbali mbali ikiwemo vifo na maradhi ya mripuko.
Aidha alisema ipo haja ya kuchukua tahadhari ya kuwahami wananchi wanaoishi hapo kutokana na ukubwa wa tatizo la athari ya kimazingira lililojitokeza katika eneo hilo hasa mmomonyoko wa ardhi uliosababishwa na matumizi mabaya ya ardhi ikiwemo ukataji wa miti ovyo.
“Kwa mujibu wa athari za kimazingira zilizojitokeza katika eneo hilo upo uwezekano wakati wowote nyumba zilizojengwa hapo zinaweza kuvunjia na nyengine kuporomoka nchini “,alisema.
Licha ya ushauri huo Mjaja aliitaka Kamisheni ya Ardhi kufanya tafiti ili kuona uhalisia wa idadi ya nyumba zinazohitajika kuondoshwa watu, ili kulinda usalama wao na mali zao.
“Kamisheni ya ardhi ishirikiane kwa karibu na Kamisheni ya Maafa ili kuhakikisha zinatumika njia sahihi katika kulinda usalama wa wananchi wanaoishi katika eneo hilo ambalo kwa mujibu wa wataalamu wa mazingira haliwezi kuendelea kuishi watu”,alisema.