NA HUSNA MOHAMMED

WANANCHI kutoka maeneo mbalimbali ya mji wa Unguja, wamepongeza uamuzi wa serikali kutoa chanjo ya kujikinga na corona kutolewa katika vituo mbali mbali vya afya Unguja na Pemba.

Walisema tamko lililotolewa na Waziri wa Afya, Ustawi wa Jamii, Jinsia na Watoto, Nassor Ahmed Mazrui, hivi karibuni walikuwa wakilisubiri kwa hamu kwani kufanya hivyo kutawafanya kwenda kuchanja bila ya usumbufu.

“Nilikuwa nasubiri kwa hamu kubwa, leo hii nimeenda Tunguu kusikiliza utaratibu wa chanjo”, alisema mmoja ya wananchi hao Khamis Fakihi mkaazi wa Jumbi alipozungumza na mwandishi wa habari hii.

Naye Hamisa Jumbe Kae mkaazi wa Fuoni, anasema kwa takribani miaka saba anaishi na ugonjwa wa kisukari hivyo anaamini chanjo ya corona itamsaidia kujikinga na ugonjwa huo.

“Nilikuwa sijui kama tayari serikali imetangaza chanjo hizo kwa wananchi lakini sasa nishajua nitatafuta njia ya kufika kuchanja”, alisema.

Kwa upande wake mchuuzi wa samaki, Issa Machano Ngwali, alisema anaona umuhimu wa kuchanja kwa kuwa hukutana na watu tofauti kwa kazi yake.

Naye Asha Salim Kingali, alisema haoni umuhimu wa kuchanja kwa sasa na kusema ni mapema mno kufanya hivyo.

“Nasubiri kwanza watu waliochanjwa nione matokeo yao halafu na mimi nitachanja lakini kwa sasa sitaki hasa kwa kuwa sina maradhi sugu na afya yangu iko vyema”, alisema.

Naye Ikram Khatibu alisema ingekuwa chanjo ya Johnson and Johnson (JJ) angalichanja kwa kuwa ni mara moja tu kuchanja lakini hii ya Sinovac ni mara mbili hivyo kwa sasa hatochanja.

Hivi karibuni, Waziri wa Afya, Ustawi wa Jamii, Jinsia na Watoto, Ahmeid Mazrui, alisema serikali kupitia wizara hiyo imeanza kutoa chanjo ya corona kwa makundi maalum hatarishi zaidi kuambukizwa ugonjwa huu ambayo ni pamoja na wafanyakazi wa milango mikuu ya kuingia nchini (viwanja vya ndege na bandarini).

Aliyataja makundi mengine ni kuwa waongoza watalii, madereva wanaosafirisha wageni na watalii, wafanyakazi wa vyombo vya usafiri vya ndani na nje ya nchi, wafanyakazi wa mahoteli, wazee kuanzia miaka 55 na watu wenye magonjwa sugu na ya muda mrefu.

Waziri huyo alisema chanjo zinazotolewa Zanzibar ni Sinovac na Sputnik Light 5 ambazo zimeanza kutolewa Juni 17, 2021 na hadi kufikia Agosti 10 jumla ya watu 9,350 wameshachanja kati yao 5,447 wamekamilisha dozi na 3,903 wanasubiri kukamilisha dozi zao.

Mazrui alitaja maeneo chanjo hiyo zinapopatikana kuwa ni katika kitengo cha kupambana na kudhibiti maradhi ya miripuko Lumumba na Hospitali ya Mnazimmoja lakini chanjo hizo zitatolewa hospitali za Kivunge, Makunduchi, Abdalla Mzee, Wete na hospitali ya wilaya Chake Chake.

Aliyataja maeneo mengine kuwa ni Micheweni, kituo cha Afya Tunguu, kituo cha Afya Fuoni na kituo cha Afya Kianga hivyo aliwaomba wananchi kujitokeza kupata chanjo kujenga kinga dhidi ya ugonjwa huo .

Kwa upande wa elimu ya afya kwa jamii, Waziri Mazrui. alisema pamoja na utoaji wa chanjo hiyo bado jamii inatakiwa kuchukua hatua za tahadhari za kujikinga ugonjwa huo ili kusaidia kupunguza kujikinga na kudhibiti kuenea kwa ugonjwa huu hapa nchini.

Aliwasisitiza, kuchukua hatua za kujikinga na ugonjwa huo kama inavyoshauriwa na wataalamu na wizara ya Afya ikiwemo kukaa umbali usiopungua mita moja baina ya mtu na mtu, matumizi ya maji salama kwa kukosha mikono au kutumia vitakasa mikono,matumizi ya barakoa,kuepuka kupeana mikono na kuepuka mikusanyiko isiyo ya lazima.​

Kwa mujibu wa wizara ya afya Zanzibar, hadi Agosti 9 mwaka huu, watu 15 waliripotiwa kufariki dunia kwa ugonjwa huyo, 390 waligundulika kuwa na maambukizi wakiwemo Watanzania 112 na wageni kutoka mataifa mbali mbali duniani 278.

Aidha wizara hiyo ilieleza kuwa kuanzia Juni 25 hadi Agosti 10 mwaka huu, watu hao 29,326 walifanyiwa uchunguzi katika vituo na hospitali mbali mbali Unguja na Pemba ambapo kati ya watu 390 waliothibitika kuwa na maambukizi, 207 walitibiwa na kupona, wagonjwa waliobaki ni 183 na wagonjwa 24 wanaendelea na matibabu.