NA MADINA ISSA
WANANCHI wa shehia zilizomo kwenye mpango wa kupatiwa chanjo ya kudhibiti maradhi ya kindupindu wametakiwa kujitokeza kwa wingi katika vituo, ili kupatiwa chanjo hiyo.
Mkuu wa kitengo cha Afya Zanzibar, Halima Khamis Ali, aliyasema hayo, alipokuwa katika mafunzo kwa waandishi yaliyofanyika katika ukumbi wa Sanaa uliopo Rahaleo mjini Zanzibar.
Alisema, zoezi la awamu ya pili linatarajiwa kuanza Agosti 11 mwaka huu ambapo wananchi watakaopatiwa ni wale waliopata chanjo hiyo awamu ya kwanza.
Aidha alisema mwananchi atakayekwenda kupatiwa chanjo hiyo ni vyema kwenda na utambulisho wa kupata chanjo awamu ya mwanzo ili kufanikisha zoezi hilo kwa awamu ya pili.
Aidha alisema ni vyema kwa wananchi kuendelea kufuata kanuni na taratibu za kinga ya kipindupindu ikiwemo ya kunawa mikono kwa maji ya kutiririka na sabuni, kuchemsha maji ya kunywa, kunywa maji safi na salama, kufunikwa vyakula ili kuzuia nzi, kuosha matunda na mbogamboga zinazoliwa bila ya kupikwa.
Alisema kwa awamu ya kwanza zoezi hilo limefanyika vizuri na ambapo wananchi walijitokeza katika shehia zilizopangwa ambapo limefikia asilimia 93.5.
Hivyo, aliwataka waandishi wa habari kuendelea kuwahamasisha wanajamii kushiriki katika zoezi la chanjo dozi ya pili ili kufikia ufanisi na lengo la kutokomeza kipindupindu ugonjwa ambao umekuwa ukiathiri sana hapa Zanzibar.
Aliwatoa hofu wananchi juu ya chanjo ya pili ya kipindupindu kwa kusema kuwa ni salama na umuhimu wa kuchukua kadi wakati wa zoezi la awamu ya pili litakapoanza.
Sambamba na hayo, Halima alifahamisha kuwa chanjo hiyo itatolewa kwa njia ya mdomo ambayo ipo kwenye mfumo wa kimiminika.
Naye, Msimamizi wa zoezi la chanjo ya kipindupindu Zanzibar, Dk. Fadhil Mohammed Abdallah, alisema wizara ya Afya, Ustawi wa Jamii, Wazee, Jinsia na Watoto kupitia kitengo cha elimu ya afya Zanzibar imelenga kumaliza kipindupindu kwa kukamilisha chanjo dozi ya pili.