NA KHADIJA KHAMIS, MAELEZO

WAZIRI wa Uchumi wa Bluu na Uvuvi,  Abdalla Husein Kombo, amewataka wahitimu wa mafunzo ya ndoa kuitumia elimu hiyo kwa kujenga subira na uvumilivu, ili kudumisha ndoa zao .

Hayo ameyasema katika Ukumbi wa  Msikiti wa Jaamiu Zinjibar Mazizini, wakati akikabidhi vyeti kwa Wahitimu wa Mkupuo wa kumi wa mafunzo ya ndoa.

Alisema lengo la kupatiwa mafunzo hayo kwa wanandoa ni kuwa walimu kwa wengine na kujenga imani subira na uvumilivu katika ndoa zao .

“Dawa pekee ya kudumisha ndoa ni kuwa na subira hasa kwa wanaume ingawa changamoto kubwa ni akinamama kukosa uvumilivu katika ndoa”alisema Waziri Kombo.

Aidha, alisema katika dini ya kiislamu imetoa miongozo mbali mbali ya kisheria kwa lengo ya kuitunza ndoa na kuipa hadhi na  heshima yake kwa kubainisha haki na wajibu kwa wanandoa.

Nae, Katibu wa Mufti,  Shekhe Khalid Ali Mfaume, amesema ameridhishwa na muamko wa wanafunzi wanaohitaji elimu ya ndoa jambo ambalo litasaidia kuepusha wimbi la talaka nchini.

Amesema mafunzo mbalimbali waliyoyapata wahitimu hao ni pamoja na maana ya ndoa kisheria, uchaguzi wa mchumba katika uislamu nafasi ya wazazi kwa wanandoa pamoja na sifa za familia ya kiislamu .

Alifahamisha kuwa licha ya mafunzo hayo wahitimu hao amefahamishwa viashiria vya migogoro katika ndoa na matokeo ya migogoro hiyo.

Nao wahitimu hao wameishukuru Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kupitia Ofisi ya Mufti  kwa kuwapatia mafunzo hayo bila ya malipo.

Walisema kuwa wataitumia elimu hiyo waliyoipata kwa vitendo kwa kujenga amani upendo na utulivu, ili kudumisha ndoa zao na kupata familia bora.