Waandishi kuibua ubadhirifu miradi ya umma

Na Zubeir H. Zubeir

Mchambuzi na Mtaalamu wa Manunuzi

HIVI karibuni Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, ilipokea taarifa ya Mdhibiti na mkaguzi mkuu wa Serikali ambapo ilionesha kasoro nyingi za matumizi ya fedha za Serikali.

Katika makala haya tutaonesha namna inavyotakiwa kuibua taarifa za manunuzi ya ovyo kwa baadhi ya miradi ya Serikali.

Vyombo vya habari vikiwa ni miongoni mwa taasisi ambazo zinatakiwa kuibua mambo mbalimbali yanayohusiana na manunuzi.

Pia kuelimisha umma kadiri iwezekanavyo kwa kufanya uchambuzi rahisi kuhusu bajeti ya serikali punde inaposomwa Baraza la Wawakilishi na kupitishwa vifungu vya matumizi.

Vyombo vya habari vinafahamu ya kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kupitia Baraza la Wawakilishi mwaka 2016 ilipitisha Sheria ya manunuzi na Uondoshaji wa mali za Uma Na. 11 2016.

Hivyo kupitia Sheria hii, Serikali imeanzisha Mamlaka ya Manunuzi na Uondoshaji wa Mali za Umma yenye jukumu la kusimamia mienendo yote ya Manunuzi katika taasisi za Umma.

Hata hivyo, moja kati ya sekta ambazo Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt. Hussein Mwinyi amekua akiizungumzia sana na kuchukizwa nayo sana katika hotuba zake ni sekta ya Manunuzi ya Umma ambayo ameonesha wasiwasi kuwa sekta hiyo ina mianya inayopoteza fedha za Umma na hasa katika uingiaji wa mikataba ambayo haileti tija kwa wananchi.

Sheria ya Ununuzi wa Umma ya Mwaka 2016 pamoja na Kanuni zake za mwaka 2020 zimeweka bayana taratibu za kufuata hadi kuingia katika mikataba, usimamizi wa mikataba na hadi kukamilika katika kufanya manunuzi ya Umma yenye tija.

Aidha, kwa kutambua umuhimu wa mikataba ya kimanunuzi katika taasisi za umma, Kanuni ya 47(1) ya Sheria ya Manunuzi Na.11/2016 imeipa  Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali nguvu ya kuhakikisha wanaipitia mikataba kwa umakini mkubwa kabla ya kusainiwa ili kuhakikisha kuwa Serikali haiingii katika mikataba ya hovyo.

Kwa mujibu wa Kanuni ya 47(1-2) ya Kanuni za Ununuzi wa Umma 2020, mkataba wowote wa aina hiyo ambao haukufanyiwa uhakiki na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali utakuwa batili (void abnitial).

Lengo kuu la kanuni hii ni kuzitaka taasisi nunuzi kabla ya kuingia mikataba na wafanyabiashara wanaokusudia kufanya kazi nao,kuhakikisha mikataba yao inaleta tija na faida kwa maendeleo ya wazanzibari.

Aidha, Kanuni ya 47(4) inaelekeza kuwa Afisa muhimu wa taasisi nunuzi anapaswa kuhakikisha kuwa ushauri wa kisheria uliotolewa na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali wakati akihakiki wa mkataba husika umezingatiwa ipasavyo na kuingizwa katika rasimu ya mkataba kabla ya kusainiwa.

Idara ya mikataba ni moja ya ofisi zilizoko chini ya Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali ambayo inashughulikia masuala yote ya kuhakiki mikataba kwa umakini ili kufahamu na kuhakikisha kuwa  taratibu za manunuzi zimefuatwa pamoja  na kutoa ushauri wa mikataba ya manunuzi ya umma kwa taasisi mbalimbali za Serikali.

Utekelezaji wa kazi za idara hii,unakwenda sambamba na matakwa ya kifungu cha 24 cha Sheria Na.6/2013 (The Attorney General’s Chambers(Discharge of Duties Act).

Idara hiyo ya Mikataba ina jukumu la kutoa ushauri wa kisheria kwa taasisi za Serikali kwa uadilifu na uweledi wa hali ya juu, kushiriki majadiliano kwa nia ya kuingia makubaliano ya kimikataba na kuhakikisha ya kuwa mikataba inayoingiwa na Serikali ina tija na manufaa kwa Taifa.

Jukumu jingine la Idara hii ni kuziangalia ibara mbalimbali za mikataba inayowasilishwa kama zimewekwa sahihi ili kuondoa uwezekano wa athari hasi kwa Serikali na kujiridhisha kama mikataba husika inakidhi au kuzingatia maslahi ya Umma au Taifa.

Hata hivyo, “chochote kizuri huwa hakikosi kasoro”, majukumu hayo yanaingiwa na changamoto nyingi kwa kuwa Idara ya Mikataba iko katika Makao Makuu ya Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali pekee, na kutokana na uchache wa watendaji uliopo,na kutokana na wingi wa mikataba inayowasilishwa, idara imekua ikichukua muda mwingi kufanya mapitio ya mikataba hio jambo ambalo inaweza kuonekana kuwa ni kucheleweshwa kukamilisha michakato ya kimanunuzi katika taasisi za Umma.

Kutokana na changamoto hiyo, Mwandishi wa Makala hii kwa kutumia haki ya kikatiba iliotolewa katika Ibara ya 18 ya Katiba ya Zanzibar 1984 kutoa mapendekezo kama Mzanzibari kuwa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa kushirikiana na maafisa masuuli wa taasisi nunuzi, imeona haja na umuhimu wa kuwajengea uwezo Mawakili wa Serikali Pamoja na maafisa sheria waliopo katika taasisi nunuzi ili Mikataba iwe inahakikiwa ipasavyo na ofisi hizo kabla ya kuwasilishwa ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali ili kupata ufanisi zaidi.

Aidha, Ili Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali itekeleze wajibu huo wa kuhakiki mikataba kwa ufanisi ipasavyo, Wizara, Taasisi na Idara za Serikali ya Mapinduzi Zanzibar zinazopeleka Mikataba katika Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali zinakumbushwa kuzingatia mambo ya msingi katika kila mkataba unaowasilishwa.

Mambo hayo ni masharti ya Kifungu cha 14(g-h) cha Sheria Na.6/2013 ya Utekelezaji wa Majukumu ya Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali inayoelekeza namna ya kupata ushauri katika Ofisi hiyo kwa kuainisha maelezo muhimu kuhusu mkataba husika.

Katika kuhakikisha kuwa Taasisi za Umma zinaingia katika mikataba yenye tija kwa wananchi na Taifa la Zanzibar,kifungu cha 14(2) cha Sheria Na.6/2013 kimetoa katazo kwa taasisi nunuzi zote kuingia katika mikataba au makubaliano ya kibiashara kabla ya mkataba husika kupata baraka kutoka Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali.


Kwa kuzingatia kwamba wanasheria wanalo jukumu la kitaaluma la kuwajibika kwa umma na kuwa walinzi makini wa maslahi ya umma dhidi ya wahujumu wa Uchumi na fedha za walipa kodi hususan kwa kuhuisha uwazi utakaoleta uwajibikaji kwenye sekta ya manunuzi ya umma, nachelelea kusema kuwa kazi hiyo inayofanywa na wanasheria haitoshi kwa sekta ya manunuzi umma ambayo huchukua zaidi ya asilimia 87 ya bajeti ya Serikali.

Ingawa zipo pia juhudi za wanasheria ambao walipelekea kuibuliwa kwa baadhi ya mambo yaliyofanyiwa kazi kikamilifu na vyombo husika.

Ipo haja ya Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali na mawakili wa Serikali wanaofanya kazi katika taasisi nunuzi “kuongeza nguvu” katika kusimamia uingiaji wa mikataba.

Utekelezaji wa mikataba hio na ufanisi unaopatikana ili kuisaidia Serikali kufikia malengo na ahadi walizozitoa kwa wananchi wakati wakiomba ridhaa kwa wananchi hao kuchaguliwa ili kuleta uwazi na uwajibikaji uliotukuka katika sekta ya ununuzi kwa wazanzibari.

Kwa kua jamii ya wazanzibari bado hawana uelewa wa kutosha juu ya umuhimu na mchango wa taaluma ya manunuzi hapa visiwani Zanzibar, sasa ni wakati ambapo wataalamu wa manunuzi.

Waandishi wa Habari na wanasheria wanapaswa kushirikiana kwa pamoja kuongeza nguvu katika kusimamia mikataba, michakato ya manunuzi na kisha kuripoti kuhusu michakato ya manunuzi ya umma na usimamizi wa mikataba husika, kuhakikisha kuna ‘uwazi’,”Ufanisi”,”Utii wa Sheria” na Ubora wa Bidhaa,Huduma au Kazi ilionunuliwa kwenye michakato ya manunuzi kama sheria ya manunuzi ya umma inavyoelekeza. Hiyo itapelekea kuokoa fedha nyingi za walipa kodi zinazopotea kutokana na kukosekana kwa uwazi unaozaa uwajibikaji.

Kwa mujibu wa ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi mkuu wa Hesabu za Serikali Zanzibar (CAG) ya Tathmini ya Utendaji kwa Mwaka wa Fedha 2019/20, kutokana na kukosekana kwa uwazi kwenye manunuzi ya umma, pamoja na mapungufu mengine ya udhaifu kwenye michakato na usimamizi wa mikataba, Serikali ilipata hasara ya kiasi kikubwa cha fedha, huku ripoti hiyo ikitaja uwepo wa viashiria vya rushwa katika michakato ya manunuzi na ukiukwaji wa matakwa ya Sheria kwa kiwango kikubwa.

Hivyo makala hii inaelezea namna wanasheria wanavyopaswa kuandaa rasimu za mikataba na kusubiria malalamiko yanayohusu utekelezaji wa mikataba au malalamiko ya madai.

Wanasheria hao wanapaswa kuhakikisha mikataba inayoingiwa na taasisi za manunuzi kuwa ni yenye tija, yenye kutekelezeka na kulingana na masharti ya jumla (GCC) na masharti maalumu (SCC) ya mikataba.

Kwa upande wa vyombo vya habari navyo vinatakiwa kuripoti matokeo haya na upotevu mkubwa wa fedha za umma na vijikite zaidi katika kutekeleza wajibu wa kuwa ‘walinzi wa mali za umma’.

Sambamba na hilo Lakini wanahabari wanatakiwa kufuatilia na kuibua harufu za ukiukwaji wa sheria ya manunuzi ya umma kwenye michakato na utekelezaji wa mikataba husika jambo ambalo litasaidia sana kuleta uwazi na uwajibikaji kwa jamii ya Wazanzibari.

Kwa bahati nzuri, Sheria ya manunuzi ya umma ya Zanzibar kifungu cha 40 kinataka michakato ya manunuzi ya umma kufanyika kwa uwazi na kwa mujibu wa taratibu pamoja na miongozo inayotolewa na Mamlaka ya Manunuzi.

Hivyo, wanahabari wanaweza kuifuatilia zabuni husika kuanzia wakati wa utangazaji wake, upatikanaji wa mshindi, namna atakavyotekeleza mkataba na ubora wa mradi husika.

Kutoa taarifa mapema za uwepo wa ukiukwaji wa sheria katika michakato ya manunuzi ya umma hupelekea Mamlaka ya Ununuzi na Uondoshaji wa Mali za Umma kuingilia kati au kusitisha mchakato, na hata kufuta mchakato, kuanzisha ukaguzi maalum dhidi ya mradi husika na kuwachukulia hatua wahusika.

Kusubiria kuandika ripoti za kufeli kwa mradi na kuchapisha katika magazeti hapa bado wanasheria na waandishi wa habari mtakua hamjaisaidia Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kupitia kalamu na taaluma walizosomea.

Katika hatua nyingine, Mamlaka ya Ununuzi Zanzibar kupitia idara ya Ukaguzi,Uchunguzi na Ufuatiliaji kwa kutambua umuhimu wa ufanisi wa utekelezaji wa mikataba na utekelezaji wa kazi za manunuzi kwa mujibu wa matakwa ya Sheria.

Hivyo, mwandishi wa Makala haya anashauri waanzishe utaratibu maalum wa kufuatilia,kuchunguza na kukagua katikati ya michakato ya manunuzi hasa katika miradi mikubwa ya Serikali kwa lengo la kuisaidia Serikali kuokoa upotevu wa fedha unaotokana na Ukiukwaji wa Sheria au usimamizi mbovu wa mikataba ya manunuzi.

Pia Mamlaka kupitia Idara ya kujenga uwezo na huduma za ushauri itumie sehemu kubwa ya bajeti yake kuhakikisha inajenga uwezo kwa taasisi nunuzi kwa ngazi zote za utekelezaji wa kazi za manunuzi.

Uzoefu katika kazi za manunuzi unaonesha kuwa maeneo ambayo yameonekana kuwa na upungufu na yanahitaji kuzingatiwa wakati wa utekelezaji kwa pande zote mbili za mkataba ni kama ifuatavyo.

Awali ni kutoteua wasimamizi wa miradi; baadhi ya miradi ilionekana kutekelezwa bila kuwapo na msimamizi aliyeteuliwa na mtendaji mkuu.

Pili; Ukiukwaji wa taratibu za mabadiliko ya mkataba; baadhi ya taasisi za umma zilimebadilika kuwa zilifanya mabadiliko ya wigo wa mkataba bila kufuata taratibu;

Aidha imebainika kuwa nyongeza ya muda wa mkataba imekuwa ikifanyika bila kuzingatia taratibu. Udhaifu huu umekuwa ukijitokeza mara kwa mara kwa kuwa wanasheria wa taasisi husika wanashindwa kusimamia ipasavyo mikataba.

Pia kutokuchukua hatua dhidi ya wazabuni wasiotekeleza masharti ya mikataba; jambo hili huisababishia Serikali hasara.

Sambamba na hilo, kuchelewesha malipo ya wakandarasi; hali hii husababisha kuongezeka kwa gharama za mikataba kutokana na riba na hivyo kuisababishia taasisi gharama.

Pia kutopeleka mikataba kwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali kuhakikiwa.

Aidha katika miradi ya ujenzi, ripoti zinaonesha kiwango cha usimamizi na utimilifu wa masharti ya mikataba ni kidogo sana

Upungufu mwingine hujitokeza katika bondi (amana) na bima za miradi ambazo huainishwa kwenye mikataba ambapo pia bima hizo haziwasilishwi kwenye taasisi husika ni mambo ya kuzingatia.

Kuchelewa kuanza kwa kazi baada ya kukabidhiwa eneo la mradi; baadhi ya taasisi nunuzi zimekuwa zikichelewa kukabidhi eneo la mradi kwa mkandarasi kwa wakati, hili huchangia katika kurefusha muda wa kazi na kuisababishia taasisi gharama zisizo na ulazima.

Aidha kutoandaliwa kwa mpango wa uhakiki wa ubora wa miradi; taasisi zimekuwa zikishindwa kuandaa mpango wa uhakiki wa mradi mara baada ya mradi kukamilika.

Jambo hili huifanya taasisi kushindwa kutambua endapo fedha iliyotumika inaendana na thamani ya mradi uliokamilika na hivyo kujikuta ikipokea mradi uliotekelezwa chini ya kiwango.

Ukosefu wa ushahidi wa kufanyika kwa mikutano eneo la mradi; baadhi ya taasisi zimekuwa hazifanyi mikutano kwenye eneo la mradi, hivyo kupelekea miradi hio kutekelezwa kinyume na taratibu na makubaliano yaliowekwa.

Pia kutokuwepo au kutozingatia ratiba ya kazi ya mkandarasi; baadhi ya miradi imekuwa ikichelewa kutekelezeka kutokana na mkandarasi kutotoa ratiba ya kazi kwa taasisi nunuzi na kujadili jinsi ya utekelezaji wa mradi husika jambo linaloweza kusababisha kuongezeka kwa gharama za utekelezaji wa mradi husika.

Sambamba na hilo, lakini malipo yenye utata kwani baadhi ya taasisi, kwa kushirikiana na wakandarasi wasio waaminifu, wamekuwa wakifanya malipo yenye utata, ambapo wakandarasi hulipwa kwa kazi ambazo hazikufanyika au ambazo hazijakamilika.

Ukamilishaji na ufungaji wa miradi; tathmini mara nyingi hufanywa kwenye miradi iliyokamilika ili kubaini ubora na utimilifu wa majengo ambapo baadhi ya miradi michoro, orodha ya maeneo yaliyokuwa na utata, utoaji wa hati ya utimilifu wa miradi, hati ya mwisho, kipindi cha matazamio, uandaaji wa taarifa ya mwisho ya kufunga mradi pamoja na malipo ya mwisho.

Pia serikali hainabudi kuandaa module ya utendaji na orodha ya matendo (Checklist) kwa kila aina ya mradi ili iwe inatoa mwongozo kwa watendaji wake, badala ya kuviziana kama ilivyo sasa.

Kama ilivyo kwa sekta nyingine, Zanzibar kuna fursa kubwa ya wanasheria kusomea masuala ya manunuzi kwa lengo la kuwa wanasheria wabobezi wa Sheria na taratibu za manunuzi ya umma sekta inayochukua asilimia 87 ya bajeti yote ya serikali.

Mwanasheria anaweza kujielemisha hata katika ngazi ya cheti au stashahada kisha kuisoma vizuri Sheria ya manunuzi ya umma, ubobezi huu utapelekea kuweka zaidi umakini na juhudi za kusimamaia katika mikataba ya manunuzi ya umma katika kuhakikisha lengo kuu la kupata thamani bora ya fedha kwenye manunuzi ya umma linafikiwa.