NA KHAMISUU ABDALLAH

WAANDISHI wa habari wameombwa kuendelea kuihamasisha jamii hasa ya kiume kupima virusi vya Ukimwi ili kupambana na ugonjwa huo hapa nchini.

Kauli hiyo ilitolewa na Mkurugenzi Mtendaji Tume ya Ukimwi Zanzibar (ZAC), Ahmed Mohammed Khatib, wakati akifungua mafunzo ya kuwajengea uwezo wanahabari juu ya kuhamasisha wanaumme kupima VIrusi vya Ukimwi katika ukumbi wa Kitengo cha Uzazi Shirikishi Kidongochekundu.

Alisema wanahabari ni wadau wakubwa katika kusaidia kuihamasisha jamii hasa wanaumme kupima afya zao mara kwa mara, ili waweze kujua afya zao na pale wanapogundulika kuwa na maambukizi na kutumia huduma za ukimwi.

Aidha alisema bado wanaumme wapo nyuma katika kupata huduma za ukimwi kutokana na kuogopa, hali ambayo inapelekea kutofikia malengo ya kupambana na maradhi hayo.

Mkurugenzi Ahmed, alifahamisha kuwa kuanzia mwezi Oktoba hadi Disemba mwaka 2020 jumla ya wanawake  31,906 wamejitokeza kupima virusi vya Ukimwi kwa Unguja na Pemba.

Alisema kati ya hao Unguja ni 26,133 ambapo 259 sawa na asilimia 0.9 waligundulika kuwa na maambukizi ya VVU huku kisiwani Pemba ni 5,773 kati ya hao 20 waligundulika kuwa na maambuki sawa na asilimia 0.3

Kwa upande wa wanaumme waliopima alisema jumla ni 25,927 kati ya hao Unguja ni 21,445 ambao waligundulika kuwa na virusi vya Ukimwi ni 152 sawa na asilimia 0.7 na Pemba ni 4,482 huku waliogundulika kuwa na maambukizi ni 17 sawa na asilimia 0.4.

Akizungumzia mambo yanayochangia wanaumme kutojitokeza kupima afya zao alisema ni pamoja na woga wa kupata majibu ya kuambukizwa, kukosekana kwa usiri katika huduma za upimani na muda mrefu wa kusubiri kupata majibu.

Sababu nyengine alisema ni mtazamo wa kuwa na tabia hatarishi katika mfumo wa maisha, kutokuwa na dalili zozote za maambukizo ya VVU na Ukimwi na kuwa na mwenza aliyepima na kuonekana hana maambukizo.