NA SALMINI SEGUMBA, (TUDARCo)

OFISA Uhusiano Bodi ya huduma ya Maktaba Zanzibar, Adila Khamis Aboud, ameitaka jamii kujiunga na uanachama wa maktaba hasa wanawake, kwani itawapa fursa za kuazima vitabu kutoka katika taasisi hiyo bila usumbufu.

Akizungumza na Zanzibar Leo, katika Ofisi za Makao Makuu ya Maktaba Zanzibar amesema wananchi wanaojiunga na Maktaba hiyo wamekuwa wakipata fursa nyingi za huduma zao zikiwemo za mtandao bila ya usumbufu wowote.

“Ukiwa mwanachama unafursa ya kuazima vitabu na kwenda navyo nyumbani kujisomea, pia fursa nyingine unaweza kutumia internet bila malipo ila ukiwa siyo Mwanachama fursa ya kuazima kitabu hutoipata ivyo utajisomea hapa hapa Maktaba na fursa ya internet bila malipo nayo utopata ni heri kuwa Mwanachama katika Maktaba ”

Pia, amesema malipo kwa ajili ya kujiunga uanachama wa Maktaba yanatofautiana, kwani watoto, watu wazima na wageni kutoka nje ya Nchi hupatiwa gharama nafuu.

Hata hivyo, Adila aliwataka wanachama wa Maktaba hiyo  kuwa makini pindi wanapoanzima vitabu kwenda navyo kujisomea nyumbani, ili kuepusha visichanike wala kuvichora ili kusaidia wengine waweze kuvuazimisha kwa ajili ya kujisomea.

Amewataka wanawake kujitokeza kwa wingi kutumia huduma za maktaba kwani imeonekana wanaume ndio wengi wanaotu eneo hilo..

Hali hiyo alisema inatokana na sehemu kubwa ya jamii bado hawajui umuhimu wa kutumia huduma za maktaba na ni vyema wakaanza  kubadilika na bodi ya taasisi hiyo itahakikisha inatoa elimu Zaidi juu ya taasisi hiyo.