NA HAFSA GOLO
MCHANGO wa maendeleo katika nchi yoyote hutegemea sana mchango wa wanawake ambao ndio kundi kubwa katika jamii nyingi hapa duniani.
Uchumi katika nchi unaposhirikisha wanawake kupewa nafasi mbalimbali za kimaamuzi na za kiutendaji, huwa ni sawa na uchumi uliojengewa mizizi imara kwani huwa kwenye mikono salama ya uendelezwa wa sekta za uzalishaji.
Katika jamii nyingi barani Afrika wanawake wamewekwa nyuma kwenye uchumu, siasa na hivyo kujikuta wakikandamizwa na kile kinachoitwa mfumo dume.
Moja ya ajenda ya serikali ya awamu ya nane inayoongozwa na Dk. Hussein Ali Mwinyi katika kujenga uchumi wa Zanzibar ni sekta ya uchumi wa buluu.
Nirahisi kuutaja uchumi wa buluu, lakini ukiuchambulia ni sekta pana nyenye matawi mengie na kufanikiwa kwake kwa hakika ni kuiona Zanzibar iliyoimarika kiuchumi na ustawi wa jamii.
Hata hivyo wakati uchumi wa buluu ukizungumzwa kama ajenda ya uchumi mpya wa Zanzibar, kuna umuhimu mkubwa kwa serikali kuwapa nafasi za kutosha wanawake kutokana na umuhimu wao.
Kwa sababu uchumi wa buluu unahusisha sekta za mafuta na gesi, hivyo mkazo lazima uchukuliwe katika kuhakikisha kama zinajitokeza fursa za masomo nje ya nchi wanawake nao wajumuishwe ili kuja kupata wataalamu wazalendo watakao simamia sekta hiyo.
Moja ya mambo alioeleza kiongozi huyo ni pamoja na kwamba imefika wakati wanawake kuhamasisha wanafunzi wa kike kujifusa kwa bidii maeneo muhimu ambayo yamehusisha uchumi wa buluu ikiwemo masuala ya mafuta na gesi,bandari,uvuvi,usafirishaji na maeneo mengine muhimu yanayogusa uchumi wa buluu.
Bila ya shaka hatua hiyo ni muhimu kwa mwanamke hasa ikizingatiwa kwamba kunahitajika matumizi ya teknelogia katika uchumi wa buluu.
Sambamba na hilo,moja ya mambo mengine muhimu yatakayopatikana ni pamoja na kuwepo kwa wataalamu wanawake ambao wataweza kusimamia masuala ya uvuvi wa kina kirefu cha maji na kutoa mchango wao kwa viwanda vitakavyowekezwa.
Ili kufikia malengo hayo kunahitajika mashirikiano ya pamoja kuwashirikisha na kuwashajihisha wanafunzi wa kike wawe na maandalizi ya kubadilisha fikra zao kiakili kwa kujiandaa na kuandaliwa kushiriki katika uchumi wa buluu badala ya kutegemea eneo la ajira ya ualimu na udaktari.
Ni wazi uchumi wa buluu utahitaji matumizi ya teknologia za kisasa hivyo wanawake watapojiandaa vyema itasaidia kutimiza malengo na kuwa chachu katika eneo hilo.
Aidha kitendo cha maandalizi mapema kwa wanafunzi wanawake kinahitajika ili wende sambamba na uchumi wa buluu.
Pamoja na hayo wazazi na walezi ni wakati wenu wa kuwatanabahisha watoto hao kujifunza kwa bidii masomo ambayo yatawezesha kutumia fursa za uchumi wa bahari.
Ni ukweli kwama kutokana na mabadiliko ya dunia ni vyema wazazi kuendelea kuwatoa watoto hao katika fikra mgando badala yake waandaliwe ili waendane na mazingira huku mkiwasimamia kufuata na kuheshimu maadili na utu wao katika suala zima la maisha na masomo yao.
Nitakuwa sijatenda haki iwapo nitakosa kuishauri serikali yangu juu ya umuhimu wa kuandaa sheria na sera ambazo zitasaidia uhamasishaji mzuri wa sekta binafsi ili waweze kuwekeza katika eneo hilo na kuongeza fursa zaidi katika eneo hilo.Hakuna lisilowezekana iwapo kila mmoja kwa nafasi yake atatumia wajibu wake.