BERLIN, UJERUMANI

WAANDAMANAJI zaidi ya 600 wametiwa mbaroni na polisi katika mji mkuu wa Ujerumani Berlin kwenye maandamano ya kupinga hatua za kufunga shughuli za kila siku zinazonuiwa kudhibiti kuenea kwa maambukizi ya virusi vya corona ambayo hayakuwa na kibali.

Maelfu ya waandamanaji walikaidi marufuku dhidi ya mandamano iliyoamriwa na mahakama na kukusanyika katika barabara za mji huo, hali iliyosababisha makabiliano na polisi.

Polisi ilisema baadhi ya waandamanaji waliwabughudhi na kuwashambulia maofisa na kupuuza vizuizi vya barabarani na hivyo kutatiza usafiri wa magari katika baadhi ya sehemu za mji huo mkuu.

Msemaji wa polisi alisema waandamanaji wapatao 5,000 walijitokeza kushiriki maandamano hayo yaliyoitishwa na vuguvugu la”Querdenker” , Watu wenye fikra za kutatua matatizo kwa njia nzuri ya ubunifu, ambalo limejitokeza kama kundi linalopaza sauti kubwa zaidi kupinga vizuizi vya corona vya Ujerumani.