NA FATUMA KITIMA, DAR ES SALAAM

WATANZANIA wametakiwa   kupuuza maneno ya upotoshaji yanayoenezwa kwenye mitandao ya kijamii kuhusu chanjo ya uviko 19 kuwa ina madhara jambo ambalo sio sahihi.

Wito huo umetolewa jana na Balozi wa Uhamasishaji wa Chanjo ya ugonjwa huo, Steve Mengele, aliewahamasisha wananchi kujitokeza na kupatiwa chanjo dhidi ya maradhi hayo.

Alieleza kuwa watu wanaoeneza uvumi kuwa chanzo hiyo ina madhara ni wapotoshaji na kwamba wanapaswa kupuuzwa kwa kuwa chanjo hiyo ni salama na imethibitishwa,

Alisema chanjo hiyo ni muhimu kwani inakusaidia kupambana dhidi ya ugonjwa huo ambao umekuwa tishio ulimwenguni hivyo kuna kila sababu kila mmoja kwa nafasi yake kujitolea kupata chanjo hiyo.

Aqidha aliwahimiza vijana kuunga mkono juhudi za serikali kwa kujitokeza kuchanja kwani wao ndio taifa la kesho hivyo wanakila sababu ya kuwekeza nguvu zao katika suala zima la kukua kwa na kuacha kuingia  kwenye makundi yasiyo na tija.

“Vijana ndio nguvu kazi ya taifa, si vyema kujiingiza katika mkumbo wa makundi yenye lengo la kuchafua serikali na kurudisha nyuma jitihada za Rais wetu (Samia Suluhu Hassan) ambaye amejikita zaidi katika kujenga uchumi na kusaida jamii kujikwamua katika wimbi la umasikini,” alieleza balozi huyo.

Naye mmoja ya wananchi waliojitokeza kupatiwa chanjo hiyo, Asha Baraka, aliishukuru serikali ya kwa kuonesha inawajali wananchi wake kwa kuwatafutia chanjo na kuigawa bure ili kuendelea kupambana na ugonjwa wa COVID 19.

Alisisitiza kwamba  ugonjwa huo upo  na unaua hivyo ni muhimu kila mwananchi katika makundi mbali mbali yenye umri kuanzia miaka 18 kujitokeza na kuchanjwa kwa hiyari ili kunusuru maisha  yao na kuwakinga ndugu, jamaa na marafiki  dhidi ya ugonjwa huo.