NA ASHURA SLIM, CHUO KIKUU HURIA

MAGARI mabovu pembezoni mwa bara bara na gereji zisizo rasmi bado ni tatizo linasababisha kuenea kwa uchafu wa mji.

Akizungumza na Zanzibar Leo, Ofisa Uhusiano wa Manispaa ya Mjini, Seif Ali Seif, alisema zoezi la uondoshaji wa magari yasiyotumika na gereji zisizotambulika kisheria, limesaidia kwa kiasi kikubwa katika  kujenga hadhi na haiba nzuri ya Mji, na  kupunguza vitendo vya kihalifu kwa baadhi ya maeneo.

Seif alisema “sote lengo letu ni moja, kujenga Nchi yetu na kuhakikisha kwamba Manispaa yetu ipo katika mazingira mazuri, uchafu si taka tu bali hata kuweka  magari mabovu ovyo zaidi ya mwaka  ni uchafu”.

Alifahamisha  baadhi ya maeneo yanayowekwa magari yasiyo tumika husababisha uhalifu, kwa kuzitumia sehemu hizo kama machaka ya kuvutia bangi hata kufanya starehe zao.

Hivyo aliitaka jamii kushirikiana kwa pamoja, ili kuondosha uchafu huo, na pindi linapotolewa agizo walitekeleze kwa wakati,  kuepusha kurejea kwa makosa hayo kwani kuna sheria maalumu ya Mwaka 2018 ya makosa ya papo kwa papo inayobainisha adhabu juu ya wasiofuata magizo ya serikali.

Alisema, tatizo la urejeaji wa uwekwaji wa  magari hayo, linasababishwa na baadhi ya watendaji wa taasisi kutokuwa waaminifu, na kutoa mianya kwa wamiliki wa gereji hizo, hivyo kupelekea kutokua na uadilifu wa utendaji kazi  na wakati mgumu kwa wasimamizi.

Aliongeza kwa  kusema , zoezi la uondoshaji magari yasiyotumika pamoja na gereji zilizokuwa hazija sajiliwa ni endelevu, hivyo ni vyema jamii ikalikubali hili kwa  kuwajibika wenyewe na kuweka mji safi.