NA MWANDISHI WETU

BODI ya Jumuiya ya Watoa Huduma katika sekta ya Mafuta na Gesi Zanzibar (ZAOGS) imekutana na kufanya mazungumzo na Uongozi wa Zanzibar Petroleum (Upstream) Regulatory Authority (ZPRA) na Kampuni ya maendeleo ya Mafuta Zanzibar (ZPDC).

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari ilieleza kuwa katika kikao hicho pamoja na mambo mengine pia kilikuwa na lengo la kuitambulisha bodi hiyo na Sekreteriati yake, na kujadiliana kwa kina namna ya kushirikiana na serikali na kuandaa warsha za pamoja zitakazotoa elimu juu ya fursa za biashara zilizopo kwenye mnyororo wa thamani katika sekta hiyo.

Mbali na hayo taarifa hiyo ilieleza kuwa kikao hicho pia kilijadili kwa kina namna ya kuelimisha na kuhabarisha wananchi juu ya viwango vya kimataifa kwa maslahi mapana ya uchumi wa wananchi wa Zanzibar na taifa kwa ujumla.

Bodi hiyo ikiongozwa na mwanzilishi na Mwenyekiti wake, Abdulsamad Abdulrahim, ililazimika kukutana na taasisi hizo ikiwa ni njia mojawapo ya kutekeleza agizo la Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi alilolitoa Disemba 5, 2020, juu ya kuanzishwa mchakato wa kuundwa kwa Jumuiya ya Watoa Huduma katika Sekta ya Mafuta na Gesi Zanzibar ili kuhakikisha wananchi wananufaika na rasilimali hizo.

Mbali na hayo taarifa hiyo ilifahamisha kwamba hatua hiyo itasaidia kuongeza ushirikiano na serikali katika kuboresha sheria zinazosimamia ushiriki wa wananchi katika sekta ya mafuta na gesi na mapato na kushirikiana na serikali katika kutengeneza na kuboresha kanuni zitakazowawezesha wananchi kushiriki kikamilifu na kunufaika na rasilimali hizo.

Sambamba na hayo taarifa hiyo ilieleza kwamba lengo lao ni kuhakikisha kwamba inatetea na kuhamasisha wananchi wananufaika na fursa mbalimbali zilizopo kwenye miradi pamoja na kuhakikisha Makampuni yatakayowekeza katika miradi mbali mbali ya sekta ya mafuta na gesi na miradi ya kimkakati inanunua huduma na bidhaa zinazopatikana nchini.