ADDIS ABABA, ETHIOPIA
KAMISHENI ya haki za Binadamu ya Ethiopia (EHRC), imesema watu wasiopungua 210 wameuawa katika ghasia na mapigano ya kikabila yaliyotokea kwa siku kadhaa katika eneo la Oromia, magharibi mwa Ethiopia.
Taarifa iliyotolewa na Tume hiyo iliwanukuu mashuhuda wakisema mapigano hayo yalianza baada ya kundi la waasi la Oromo Liberation Army (OLA) kuwasili katika mji wa Gida-Kirimu jimboni Oromia mnamo Agosti 18, kufuatia kuondoka askari wa serikali katika eneo hilo la magharibi mwa Ethiopia.
Wakaazi wa eneo hilo waliiambia EHRC kuwa, watu zaidi ya 150 wameuawa na wapiganaji wa genge hilo linalodai kupigania ukombozi wa watu wa jamii ya Oromo.
Habari zaidi zinasema kuwa, kufuatia mauaji hayo, wimbi la mapigano ya kulipiza kisasi lilijiri katika eneo hilo na kupelekea watu wengine 60 kuuawa.
Hata hivyo, kamisheni hiyo ya serikali haijasema ni nani waliohusika na mauaji hayo ya ulipizaji kisasi.
Kundi hilo la OLA linakadiriwa kuwa na wapiganaji wapatao 2,800 kwenye sehemu za magharibi na kusini mwa mkoa wa Oromia.
Makundi ya waasi katika eneo hilo yanadai kupigania haki za Waoromo ambao ni asilimia 35 ya watu milioni 110 wa Ethiopia.
Haya yanajiri wakati ambapo eneo la Tigray la kaskazini mwa nchi nalo linakumbwa na mapigano na uasi unaoongozwa na kundi la wapiganaji la TPLF.