NIAMEY, NIGER

TAKRIBAN watu 55 wamefariki dunia kufuatia janga la mafuriko nchini Niger huku 34 wakijeruhiwa na maelfu wakipoteza nyumba na makaazi yao.

Mafuriko hayo yalitokea baada ya mvua kubwa kunyesha katika mji mkuu Niamey, na kusababisha uharibifu mkubwa wa mali na roho za watu.

Zaidi ya nyumba 4,000 na vibanda 200 vilianguka na mifugo 800 ilisombwa na maji, kulingana na ripoti ya Ufuatiliaji wa Huduma ya Ulinzi wa Raia.

Mikoa kadhaa nchini Niger imeathiriwa vibaya na mafuriko ambayo yamekuwa yakitokea tangu mwanzoni mwa mwezi Juni mwaka huu.

Mji mkuu ni miongoni mwa miji iliyoathiriwa zaidi  na mvua ya milimita 144 iliyorikodiwa.

Serikali ya Niger ilitangaza kuwa, zoezi la uokoaji na utoaji misaada linaendelea licha ya kuweko changamoto nyingi.

Baadhi ya raia wamekwama katika baadhi ya maeneo kutokana na kutokuweko mawasiliano kutokana na barabara kutopitika katika maeneo hayo.

Aidha katika baadhi ya miji madaraja yalibomolewa na mafuriko sambamba na kukatika mawasiliano ya simu na kukosekana huduma za maji na umeme.

Niger ni miongoni mwa nchi ambazo hukumbwa na janga la kimaumbile la mafuriko kila mwaka na kusababisha mamia ya watu kupoteza maisha.