RIYAD, SAUDI ARABIA

SHIRIKA la kimataifa la kutetea haki za binadamu la Amnesty International limesema idadi ya matukio ya utekelezaji wa hukumu ya kifo nchini Saudi Arabia imeongezeka.

Ongezeko hilo ni baada ya nchi hiyo kukamilisha muda wa urais wa kundi la nchi zilizostawi na zinazoinukia kwa kasi kiuchumi duniani za G20 mnamo Disemba mosi mwaka uliopita.

Katika ripoti yake iliyochapishwa shirika hilo limesema kati ya mwezi Januari na Julai mwaka huu watu 40 walinyongwa.

Idadi hiyo ni kubwa zaidi kuliko 27 walionyongwa mwaka mzima wa 2020 wakati Saudi Arabia ilipokuwa rais wa G20.

Naibu Mkurugenzi wa Amnesty International Mashariki ya Kati na Afrika Kaskazini Lynn Maalouf alisema mara tu kuangaziwa kwa Saudi Arabia na G20 kulipofifia mamlaka za ufalme huo zilianza tena kuwaandama watu waliotoa maoni yao kwa uhuru au kuikosoa serikali.