NA KHAMISUU ABDALLAH

WATU 18 wamefikishwa katika mahakama ya mwanzo Malindi kwa tuhuma za kufanya biashara ya vileo bila ya kuwa na leseni.

Washitakiwa hao ni Rose Shayo Shayo (24), Naima Hussein Khamis (27), Maryam Samuwel Kikungwa (30) wote wakiwa wakaazi wa Chukwani na Johari Ali Ismail (25) mkaazi wa Mpendae.

Wengine ni Milan Habibi Mgeni (30) mkaazi wa Amani, Salma Omar Kimeta (28) mkaazi wa Fuoni, Neema Galson Kahaya (31)mkaazi wa Darajabovu, Leluu Omar Said (26) mkaazi wa Bububu na Meri Elias Njai (29) mkaazi wa Dunga.

Wengine ni Pendo Gastor Kihaka (26) mkaazi wa Amani, Laura Remi Marandi (46) mkaazi wa Bububu, Ali Hussein Ali (28) mkaazi wa Kiembesamaki na Juma Helman Magozi (43) mkaazi wa Amani Fresh.

Mbali na washitakiwa hao wengine ni Deo Makweba Sylvester (30) mkaazi wa Amani, Doto Cosmas Joseph (42) mkaazi wa Darajabovu, Peter James Manyai (35) mkaazi wa Kijangwani, Endru Emanel Pana (46) mkaazi wa Mwakaje na Peter Bonifase Bayo (26) mkaazi wa Magogoni wilaya ya Magharibi ‘B’ Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja.

Wakiwa mahakamani hapo mbele ya Hakimu Mwanaidi Abdalla Othman washitakiwa hao walisomewa shitaka lao na Mwendesha Mashitaka wa mahakama hiyo Suleiman Khalfan Masoud.

Wote kwa pamoja walishitakiwa kwa kosa la kufanya biashara ya vileo bila ya kuwa na leseni kinyume na kifungu cha 45 (1) (2) na kifungu cha 49 kifungu cha adhabu sheria ya mwaka 2020 sheria za Zanzibar.

Mwendesha Mashitaka aliwasomea mashitaka yao mmoja mmoja ambapo walidaiwa kuwa Agosti 22, mwaka huu, majira ya saa 3:00, saa 4:00 na saa 5:30 usiku, walikamatwa katika baa mbalimbali za mkoa wa Mjini Magharibi wakiwa wanafanya biashara ya vileo kwa kuuza bia aina ya Serengeti, Stle lite, safari, Kilimanjaro, balini, henken na Prizna.

Wote hao, walikamatwa katika baa mbalimbali ikiwemo Chukwani, Amani, Kisauni, Gymkana, Magogoni, Amani kwa Mbawala.

Washitakiwa hao waliposomewa shitaka hilo walilikataa huku mshitakiwa Rose Shayo, alikubali kosa lake na kuiomba mahakama impunguzie adhabu na kuahidi hatorejea tena.

Hakimu Mwanaidi alimtia hatiani mshitakiwa huyo na kumuona ni mkosa kisheria na kumpa adhabu ya kulipa faini ya shilingi 1,000,000 na akishindwa atatumikia Chuo cha Mafunzo kwa muda wa miezi sita.