NA MWANAHAWA HARUNA (SCCM)

WAZEE katika Nyumba za kutunza Wazee Sebleni wamesema wanafurahishwa na huduma zinazotolewa katika kituo hicho  kwa kuwapatia wafanyakazi wanaowajali katika kuwapatia huduma zao.

Kauli hiyo, wameitowa wakati walipokuwa wakihojiwa na Zanzibar Leo huko Amani Mjini Unguja,  ambapo Asaa Ali Issa alisema wamekuwa wakipata ushirikiano mkubwa kutoka kwa walezi hao hao jambo linawapa faraja ya kuishi kwa Amani.

Alieleza kuwa licha ya kuwa wanalelewa kituoni hapo wanajihisi wapo nyumbani na kuwashukuru Maraisi wote ambao wameiongoza Zanzibar kwa awamu zote kwa kuweza kuwakumbuka wazee hao na kuwapa kipao mbele.

“Tunapewa kila mwezi 40,000 na kati ya kila mwezi tunapewa pencheni ya elfu 20,000 kula tunakula kwa wakati na kila ifikapo skukuu tunapata nguo kutoka kwa serekali na tunapelekwa safari tofauti hatuna shida bali tuwashukuru viongozi wetu,”alisema.

Aidha alisema kuwa, hawanabudi kuwashukuru viongozi wa nchi hususani muasisi wa Zanzibar marehemu Shekh Abeid Amani Karume, kwa kuwaza kujenga mahali ambapo wazee wanapata faraja katika maisha yao.

Nae, Mtoro Seif Hija, amefahamisha kuwa wanapata matibabu bure na pindi tu wanapojihisi vibaya haraka hupelekwa Hospitali na bila ya gharama yoyote.