NA LAYLAT KHALFAN

WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa, Serikali za Mitaa na Idara Maalum za SMZ, Masoud Ali Mohammed, amewaagiza maofisa mapato kukusanya kodi kwa kutumia mashine za kielektroniki ili kudhibiti mianya na upotevu wa fedha za umma.

Waziri huyo aliyasema hayo wakati akikabidhi mashine 75 za kielektroniki za kukusanyia kodi kwa wakuu wa mikoa mitatu ya Unguja, kwa lengo la kudhibiti mapato.

Alisema kwa kipindi kirefu kumekuwa na upotevu mkubwa wa mapato ya serikali kutokana na ukusanyaji kodi kwa njia ya mkono.

Aidha, waziri Masoud alisema ana imani mashine hizo zitasaidia kwa kiasi kikubwa kuepusha tatizo hilo ambalo limekuwa likiathiri uchumi wa nchi siku hadi siku.

“Uvujaji mapato sasa basi naamini nchi yetu itakuwa na maendeleo kwa kuwa kifaa cha kukusanyia mapato kimepatikana hususan kwa mabaraza yetu”, alisema.

Aidha alifahamisha kuwa serikali itaendelea kuchukua jitihada za kudhibiti upotevu wa mapato kwa lengo la kujiimarisha kiuchumi na kufikia maendeleo.

Wakati huo huo waziri Masoud alifungua mafunzo ya mfumo wa usajili wa wajasiriamali wadogo katika ukumbi wa kikosi cha Valantia Mtoni na kuwataka maofiza kodi wa mabaraza ya miji na manispaa kutoa taarifa kwa wakuu wa mikoa wanapokwenda kukusanya kodi katika maeneo yao.

Mapema Mkurugenzi wa Kampuni iliyotoa mafunzo hayo AIM Group Limited kutoka Tanzania bara inayojishughulisha na utengenezaji wa mifumo ya kidigitali Paul Bomani, alisema kitambulisho hicho kitamuwezesha mjasiriamali kutambulika na kurahisisha ulipaji kodi.

Alisema kwa sasa kitambulisho hicho kishaunganishwa na mfumo wa malipo wa serikali ZAN Malipo kwa lengo la kurahisisha upatikanaji wa huduma hiyo.

“Niwaombe mnaohusika na masuala ya kodi hakikisheni kila mjasiriamali anapata kitambulisho chake hii itawarahisishia ukusanyaji wa mapato na taifa litaimarika kiuchumi na kusonga mbele”, alisema.