NA HAFSA GOLO

WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Rais Katiba,Sheria na Utawala Bora, Haruoun Ali Suleiman amesema serikali inasisitiza kwamba mapendekezo au mageuzi ya mabadiliko ya sheria lazima yazingatie  kwa umakini mila na desturi za Mzanzibar.

Katibu wa Madili ya Utumishi wa Umma, Asma Haji Jidawi alieleza hayo kwa niaba ya Waziri huyo, wakati alipokuwa akifungua mkutano wa siku tatu wa wadau wa masuala ya sheria wenye dhamira ya  kujadili sheria kandamizi kwa mama wajane Zanzibar uliofanyika ukumbi wa Mtakwimu Mkuu wa Serikali Mazizini.

Alisema lengo ni kuhakikisha mapendekezo yatakayowasilishwa serikalini yanatekelezeka na sio kuleta mzozo au mjadala mwengine kwa sababu ya kwenda kinyume na mila na silka za Mzanzibar.

Aidha alisema jambo jengine linalosisitizwa ni pamoja na kuhakikisha fursa za kiuchumi kwa wajane na wanawake wenye kuishi mazingira magumu na watoto zimewekwa bayana na bila ya kuleta vikwazo katika utekelezaji wake.

“Mapendekezo  hayo, vile vile  yazingatie fursa za elimu maalumu ili wanawake waweze kulea watoto wao katika mazingira yenye msingi wa elimu kwani maendeleo yanaletwa kwa elimu na fedha na sio fedha peke yake”,alisema.

Alifahamisha kwamba misingi yote hiyo  inalenga kuleta mabadiliko ili wanawake wajane ,wanawake wanaoishi mazingira magumu na watoto waweze kupata fursa muhimu ikiwemo malazi ,chakula ,nguo pamoja na kupunguza wimbi la talaka zinazoenda kujitokeza ndani ya jamii.

Nae Mrajisi wa Asasi za Kiraia zisizo za Kiserikali, Ahmeid Khalid Abdulla, alisema ni vyema Jumuiya ya Wajane Zanzibar (ZAWIO) iwe mstari wa mbele kupinga vitendo vya udhalilishaji huku ikihakikisha inaendesha na kusimamia mambo yake  kwa misingi  na taratibu za nchi.

Aliwataka watakapojadili sheria lazima waangalie mahitaji ya kinamama na watoto, ili yasiwe kandamizi sambamba na kuleta maendeleo endelevu katika maisha yao.

Alifahamisha kwamba serikali ya Mapinduzi Zanzibar ipo pamoja na jumuiya hiyo katika kuhakikisha changamoto zinazowakabili wanawake wajane zinapatiwa ufumbuzi pamoja na fursa na haki za watoto zinachukua nafasi yake.

Katibu wa Tume ya Kubadilisha Sheria Zanzibar,Mussa Kombo alisema tume hiyo ina jukumu la kubadilisha sheria kwa kuzingatia katiba,mikataba ya kimataifa pamoja na maslahi mengine muhimu.

Hivyo alisema katika sheria yapo mambo ambayo yanakwaza ndani ya sheria na yanahitaji marekebisho na mengine yanahitaji elimu.

Alibainisha miongoni mwa sheria nyengine inayohitajika kupitiwa ni pamoja na sheria ya kulinda wari ambayo kwa sasa imekuwa na mtanganyiko katika utekelezaji wake.

“Sheria hiii wadau lazima ipitiwe upya ili iweze kulinda haki za watoto wote”,alisema.

Kwa upande wa Mkurugenzi wa Jumuiya ya Wajane Zanzibar, Tabia Makame Mohammed, alisema kwamba sheria bado hazijaweka bayana haki za wanawake wajane,   jambo ambalo linaendelea kukandamiza  haki za watoto na kuendelea kuathirika na mazingira ya kiuchumi na kijamii.

Alisema idadi kubwa ya watoto wamekuwa wakikosa haki zao kutokana na sheria kuwa rafiki ama wasimamizi wa sheria hawatimizi majukumu yao ipasavyo.

“Kama sheria zipo kwa nini tassisi husika inashindwa kusimamia ili watoto wapate haki zao za msingi baada ya ndoa kuvunjika ama mzazi mmoja kupoteza maisha tumekuwa tukishughudia mambo mbali mbali yakijitokeza ndani ya jamii ambayo yanakandamiza haki za watoto na kuendelea kunyanyasika “,alisema.