NA HAFSA GOLO

WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Idara Maalumu za SMZ, Masoud Ali Mohamed, amewataka wafanyakazi kuishi maisha ya utumishi wa umma kwa kuzingatia miiko ,maadili  na kanuni zinazoongoza masuala ya utumishi wa umma.

Aliyasema hayo wakati alipokuwa akizungumza na gazeti hili ofisini kwake Vuga mjini Unguja.

Alisema amebaini bado wapo  baadhi ya wafanyakazi hasa katika serikali za mitaa na upande wa usajili wa matukio ya kijamii hawajafahamu wajibu wao wa majukumu ya kiutendaji badala yake wamekuwa wakipuuza miiko ya maadili ya utumishi wa umma.

Aidha Waziri huyo alisema maisha hayo hayawezi kuvumilika wala kufumbiwa macho hasa ikizingatiwa serikali ya awamu ya nane inahitaji ufanisi na uadilifu katika utoaji wa huduma.

“Nawasihi wafanyakazi katika taasisi hizo waendelee kubadilika zaidi, ili kufikia malengo ya serikali ili huduma zinazotolewa ziondokane na urasimu na rushwa mambo ambayo hayakubaliki kisheria katika utawala bora”,alisema.

Hivyo Masoud, aliendelea kuwahimiza watendaji kufanya kazi kwa kufuata sheria namba 2 ya utumishi wa umma ya mwaka 2011, sambamba na kuepuka rushwa na ubadhirifu  na matumizi mabaya ya fedha za umma.