NA HAFSA GOLO
SERIKALI inaendelea kutafuta wawekezaji wa ndani na nje ambao watasaidia kukamilisha ujenzi wa miradi ya maendeleo katika masoko na maegesho nchini.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Idara Maalum za SMZ, Masoud Ali Mohammed, alieleza hayo alipokuwa akizungumza na mwandishi wa habari hizi ofisini kwake Vuga mjini Unguja.
Alisema miradi ya maendeleo ambayo inayotaka kukamilishwa ipo tisa ikiwemo masoko matano, na vituo vya maegesho vinne.
Aidha alisema ndani ya miradi hiyo kutakuwa na ujenzi wa vituo viwili vya mabasi ambacho kimoja kitajengwa Chuini kisiwani Unguja na chengine Kangajani kisiwani Pemba.
“Mbali na miradi hiyo tutajenga maegesho katika maeneo mbali mbali ikiwemo eneo la Malindi mjini Unguja”,alisema.
Alisema kukamilika kwa ujenzi wa miradi hiyo kutasaidia mji wa Zanzibar kuwa na haiba nzuri sambamba na kuimarisha matumizi mazuri na kuondoa changamoto kwa watumiaji wa maeneo hayo.
Aidha alisema katika utekelezaji wa hatua hiyo Ofisi hiyo tayari imeshafanya upembuzi yakinifu ambao umeshatenga maeneo rasmini na kujua gharama ya kila ujenzi ingawa ilikuwa ni mapema kuweka wazi.
“Serikali imedhamiria kuleta mabadiliko ya maendeleo Zanzibar kwa kutekeleza miradi mbali mbali ya maendeleo jambo la msingi kwa viongozi na watendaji kutimiza wajibu wao ipasavyo hasa ikizingatiwa suala hilo linamgusa kila mwananchi”,alisema.
Wakati huo huo alisema, hivi karibuni Ofisi hiyo inatarajia kufanya majaribio ya uzalishaji katika miradi ya viwanda iliyotekelezwa na Idara Maalum ya SMZ.
Alifahamisha kwamba lengo ni kuona mwenendo mzima wa miradi hiyo inavyoweza kuleta uzalishaji wenye tija na kufikia malengo yaliokusudiwa ikiwemo kupunguza gharama kubwa kwa serikali kuagiza bidhaa za watendaji wa idara hivyo ambazo zinaweza kuzalishwa Zanzibar.
“Tunatarajia kufanya majaribio katika kiwanda chetu cha viatu ambacho bidhaa hizo zitatumika katika soko la ndani na la nje”,alisema.
Waziri huyo alitumia nafasi hiyo kutoa wito kwa wananchi kuunga mkono juhudi za serikali yao huku wakitambua kwamba hayo ni miongoni mwa mafanikio.
Alisema hatua hiyo iwe sambamba na kuunga mkono juhudi za Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Hussein Ali Mwinyi katika mapambano dhidi ya rushwa ubadhirifu wa matumizi mabaya ya fedha za umma.
Aliwataka wananchi kutambua kwamba serikali ina malengo na dhamira ya dhati katika kuleta mabadiliko ya kiuchumi na kijamii hivyo imekuwa mstari wa mbele kupiga vitendo vinavyochangia kufikia mafanikio kwa wakati.
“Rushwa, urasimu na matumizi mabaya ya fedha za umma ni miongoni mwa vichocheo vinavyochangia kuduma za maendeleo nchini hivyo sote kwa pamoja tupinge kwa nguvu changamoto hizo”,alisema.