KUALA LUMPUR, MALAYSIA

WAZIRI  Mkuu wa Malaysia Muhyiddin Yassin amepuuza shinikizo linaloongezeka la kumtaka ajiuzulu, akisema kuwa bado ana uungwaji mkono mkubwa miongoni mwa wabunge na atathibitisha hilo wakati bunge la taifa hilo la Kusini mashariki mwa Asia litarejea mwezi ujao.

Kwenye hotuba kupitia televisheni, Muhyiddin alisema Mfalme Al-Sultan Abdullah alikubali kuwa abaki madarakani kukisubiriwa kura hiyo ya imani, ingawa baadhi ya viongozi wa serikali yake ya muungano hawamuungi mkono.

Shinikizo la kumtaka kuondoka liliibuka tena wiki iliyopita, baada ya mfalme kutoa tamko la nadra la kuikemea hatua ya serikali kutangaza sheria za hali ya dharura bila idhini yake, kitendo ambacho uongozi wa kifalme ulisema kinakwenda kinyume na katiba.

Chama cha United Malays National Organization, ambacho ndicho kikubwa kabisa katika muungano unaotawala, kilisema Muhyiddin alipoteza uhalali baada ya tamko la mfalme.