NA HUSNA MOHAMMED
WIZARA ya Afya, Ustawi wa Jamii, Wazee, Jinsia na Watoto Zanzibar, imesema itaanza kutoa chanjo ya corona kwa watu wenye maradhi sugu mara baada ya utaratibu kukamilika.
Akizungumza na gazeti hili, Mkuu wa Kitengo cha Kinga, katika wizara hiyo, Halima Ali Khamis, alisema kuwa watu wenye maradhi kama, kisukari, moyo, presha, saratani, maambukizi ya UKIMWI na mengine sugu watapatiwa chanjo hiyo kwa hiari.
“Hawa wote wako katika hatari kubwa ya kuugua na wakipata corona ni rahisi kupoteza maisha hivyo tunalenga kuwapa chanjo hawa na baadae kufuata makundi mengine”, alisema.
Aidha alisema katika chanjo hizo pia wamelenga kwa wananchi walioanzia miaka 45 na kupindukia kupatiwa chanjo hizo kwa kuwa baadhi yao kinga zao za mwili zimeshaanza kushuka.
Mkuu huyo wa kitengo aliongeza kuwa sambamba na makundi hayo lakini pia alisema wanakusudia kutoa chanjo hiyo kwa wafanyakazi wanaohudumia watu wengi kama walimu wa skuli na madrasa, viongozi wa dini kwa maana misikiti na makanisa, mabenki, uwanja wa ndege, bandarini, mahospitalini na kadhalika.
“Tayari tumeanza na wahudumu wa afya, bandarini, uwanja wa ndege na wananchi wanaoenda nje ya nchi kwa zile chanjo za awali 100,000 na zoezi hili litaendelea kwa wananchi ambao watataka kuchanjwa wakati chanjo nyengine zikiwasili wakati wowote kuanzia sasa”, alisema.
Hata hivyo, alisema wizara imeandaa utaratibu wa utoaji wa mafunzo maalumu kwa wanajamii, viongozi wa dini, wanasiasa na makundi mengine juu ya umuhimu wa chanjo hiyo.
Alisema kuna baadhi ya watu wamekuwa wakipotosha kwa njia moja au nyengine jambo ambalo halina uhakika wowote na hivyo kuwatia hofu wenye nia ya kutaka kuchanja chanjo hiyo.
“Hao wote waliochanjwa hadi sasa hakuna tatizo lililojitokeza na wengine washakamilisha dozi zote mbili tunawataka wananchi walio tayari wakati ukifika kujitokeza kwa wingi”, alisema.
Alisema Zanzibar inatarajia kupokea dozi ya chanjo ya Sinovic kutokea China na taratibu nyengine juu ya utoaji wa chanjo hiyo kwa wananchi utatolewa baadae.