MOGADISHU, SOMALIA

SHIRIKA la Mpango wa Chakula la Umoja wa Mataifa (WFP) limetangaza kuwa, linahitaji zaidi ya dola za Marekani Millioni 210 kuwasaidia wakimbizi hao wa ndani kupata chakula ifikapo mwezi Desemba.

Fatuma Nishow mmoja wa wakimbizi wa ndani wa Somali alisema hawajapika chakula kwa siku nne zilizopita, kwa sababu hakuna chakula,wanakabiliwa na njaa na wanahitaji msaada wa haraka.

Khadija Muhammad Diriye, Waziri wa Somalia wa Masuala ya Misaada ya Dharura na Majanga alisema hao ni wakimbizi wa ndani wanaokabiliwa na changamoto nyingi.

Walilazimishwa kutoroka makwao ambako waliishi kwa miaka mingi na ambako walizalisha mazao yao ya chakula, sasa hawana mahali pa kuishi.

Pia kuna chakula kidogo sana kutokana na vikwazo vya barabarani. Maji ni kidogo mahitaji ya kila siku ndiyo changamoto kubwa kwa wakimbizi hao.

Naye Olga Cherevko,mwakilishi wa shirika la kutoa misaada la Umoja wa Mataifa, anahofia ongezeko la wakimbizi wa ndani litasababisha hali kuwa mbaya zaidi.

Uhaba huu wa  chakula nchini Somalia, umechangiwa na  ukame, mafuriko, uvamizi wa nzige na pia kuzuka wa gonjwa la Covid-19 katika majimbo ya Somali land na Puntland.

Somalia ilitumbukia katika vita vya wenyewe kwa wenyewe mwaka 1992 baada ya kuangushwa utawala wa Siad Barre.

Katika miaka ya hivi karibuni nchi hiyo imeshuhudia kuongezeka kwa hujuma za magaidi wa al-Shabab na hivyo kuwasababishia raia wa nchi hiyo matatizo makubwa.