BEIJING, CHINA

JUHUDI za kuchunguza vyanzo au chimbuko la virusi vya corona ambavyo hadi sasa vilisababisha vifo vya mamilioni ya watu na kulemaza chumi za mataifa ulimwenguni, zimesimama, huku muda ukizidi kuyoyoma.

Hayo yalisemwa na wanasayansi waliotwikwa jukumu na Umoja wa Mataifa la kuchunguza chanzo cha virusi hivyo.

Katika taarifa yao,walisema kadri muda unavyosonga, ndivyo uchunguzi wa chimbuko la virusi hivyo vilivyoripotiwa mwanzo Wuhan nchini China mwishoni mwa mwaka 2019 unazidi kuwa mgumu huku ushahidi ukitoweka au kuharibiwa.

Taarifa hiyo imejiri chini ya wiki mbili tangu Shirika la Afya Duniani WHO lilipoihimiza China kutoa habari kuhusu visa vya mwanzo vya corona.

Ripoti ya awali iliyotolewa na wataalam wa kimataifa waliotumwa nchini China na WHO mwezi Januari, kuchunguza chimbuko la virusi hivyo, ilisema kulikuwa na uwezekano mkubwa kwamba virusi hivyo vilitoka kwa popo hadi kwa wanadamu.