NA MWANDISHI WETU

IKIWA waislamu kote ulimwenguni wako katika shamrashamra ya kuusherehekea mwaka mpya wa kiislamu 1443, ni vyema kwa muislamu ajue lini mwaka huu ulianza na kwa nini uliitwa mwaka wa hijra.

Mwaka mpya wa kiislamu kwa hapa Zanzibar sio wengi ambao wanautilia maanani kiasi kwamba wako baadhi ya watu hawajui hata lini mwaka mpya wa kiislamu licha ya kuwa idadi kubwa ya wazanzibari ni wasilamu.

Kabla ya hijra (Mtume kuhama kutoka Makka kwenda Madina) waislamu walikua wakijua tarekhe zao kupitia kuzaliwa kwa Mtume mfano, Sayyidina Uthman alizaliwa mwaka wa 6 baada ya kuzaliwa Mtume baada ya mMume kupewa utume wakaanza kuhesabu tarekhe kwa kutimilizwa kwake ambapo Sayyidina Omar alisilimu mwaka wa 5 baada ya Mtume kutimilizwa.

Na kabla ya hapo walikuwa wakizijua tarekhe kwa kutumia mwaka wa miladia yaani tangu kuzaliwa Nabii Issa (A.S), Nabii Mohammad alizaliwa mwaka 571M tangu kuzaliwa Nabii Issa (A.S).

Ama miezi hii ya muandamo muhrram mpaka dhul hijja, hii ilikuwepo toka Mwenyezi Mungu alipoumba mbingu na ardhi na  idadi yake kama Qur’an inavyotueleza ni 12 (qur’an 9:36).

Ila tu haikujulikana kama sasa tuko mwaka wa ngapi na ndiyo maana ikajulika tu kihistoria kwamba Mtume alizaliwa mwezi wa Rabi’unil aw wal (mfunguo sita) ambao ni mwezi wa tatu kwa utaratibu wa kalenda ya kiislamu kama tutakavyoona.

Mwezi wa kwanza ni muhar ram, wa pili ni swafar  wa tatu ni Rabi’unil aw wal, wa nne ni Rabi’unith thaani, wa tano ni Jumaadal ulaa, wa sita ni Jumaadath thaania, wa saba ni Rajab, wa nane ni Sha’aban, wa tisa ni Ramadhani, wa kumi ni Shaw waal, wa kumi na moja ni Dhul qi’da, na wa kumi na mbili ni Dhul hujjah.

Mtume alizaliwa katika mji wa Makka tarekhe 12/3 (mfunguo sita) siku 50 baada ya tukio la kuangamizwa Abraha (al ashram) pamoja na Jeshi lake (watu wa tembo) ambao tangu kuzaliwa Nabii Issa (A.S) ulikuwa ni mwaka wa 571 miladia.

Aliishi Makka Mtume  ( baada ya kupewa utume akiwa na umri wa miaka 40) kwa muda wa miaka 13 kisha akaamrishwa kuhamia Yathrib ambayo baadaye na mpaka sasa inaitwa al madinatul munaw wara.

Baada ya kuhamia Madina Mtume aliishi  kwa muda wa miaka 10 kisha akafariki dunia ikiwa bado waislamu hawajawa na hesabu ya mwaka huu wa kiisilamu.

Hivyo basi, ulipofika mwaka wa 17H katika khilafa ya Sayyidina Omar ndipo fikra za tarekhe zikaanza.

Alisema A.S Sayyid Abdur rahman as suhailiy (katika ar raudhul unuf) Maswahaba walianza kuhesabu tarekhe kutokana kauli ya Mwennyezi Mungu aliposema (min aw wali yaumin) (qur’an 9:108) kwa sababu inavyojulikana sio siku ya mwanzo kwa kukata bali ni siku ya mwanzo ambayo uislamu ulipata nguvu na Mtume akaweza kumuabudu Mola wake kwa amani bila misukosuko yoyote.

Mwaka wa Hijra ni mwaka ambao Mtume (SAW) pamoja na maswahaba waliihama ardhi ya SHIRKI (Makka) kutafuta nusra ya Mola (Madina).

Hijra ilitenganisha baina ya haqi na batwil, Hijra ilidhihirisha ushindi kwa uislamu na waislamu ambapo Mtume na maswahaba wakaweza kumuabudu Mola wao kwa amani kama tulivyo eleza hapo awali.

Baadaye likazuka swali la pili kuhusu ni mwezi gani uwe wa kwanza? Rai pia hapa ziligongana wengine wasema tuanze na Ramadhani, wengine tuanze na rabi ‘unil aw wal (mfunguo sita) wengine tuanze na rajab lakini mwisho ikaafikiwa rai ya say yidina Ali kuanza na mwezi wa muharram kwa sababu zilizo kuwa na uzito kama ifuatavyo;

Ni mwezi ambao mahujaji wanarudi kutoka hijja, ibada iliyowafanya kusamehewa madhambi yao yote wakarudi kama walivyo zaliwa hawana kosa hata moja.

Kwa sababu hiyo kwamba wanaanza upya kuchuma na mwezi unao andama baada ya dhul hijja ambao ni muhar ran ni mwezi wa kwanza katika mwaka (mwaka mpya)
Lengo na maazimio ya Mtume kuhama yalianza katika mwezi wa muharram pamoja na kuwa safari ya hijra ilikuwa rabi’unil aw wal (mfunguo sita)

Mwaka huu wa Hijra waislamu ndio mwaka ambao kila muislamu katika pande zote za ulimwengu ana haki ya kuutambua, kuupa hadhi na kuusherehekea.

Lakini utaona wengine hawautilii maanani wakisubiria mwaka mpya WA kidunia ambao hauwahusu na kibaya zaidi hawaujui maana yake nini.

Kuusherehekea mwaka huu ni dhambi kubwa kwa waislamu, na sasa tuamkeni kwa kuwa hijra kama ambavyo ina maana ya kuhama kutoka eneo kwenda jengine, aidha ina maana ya kuyahama maaswiya na kuingia katika twa’a.

Tuipatilize fursa hii kwa sababu hatuna uhakika kama mwakani tutafika, au tutafika, lakini je, tutakuwa na afya ya kutuwezesha kufanya mema? Ukiiona asubuhi usidhani jioni utafika na ukiiona jioni usitazamie kuipata asubuhi.

Tujiulize waislamu, mangapi tumeyafanya katika mwaka huu ulio (tumaliza kama sikuumaliza) yanayomuudhi Mwenyezi Mungu? Turudi katika kumtii Allah ili tuepukane na fedheha za duniani na adhabu iumizayo siku Qiyama

Tunawatakia waislamu wote kote ulimwenguni mwaka mpya wa kiislamu.