NA LAYLAT KHALFAN

WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa Serikali za Mitaa na Idara Maalum za SMZ, Masoud Ali Mohammed, amesema ofisi yake imepanga mikakati ya kukabiliana na mapungufu iliyojitokeza katika kipindi kilichopita, ili kuziimarisha zaidi taasisi zilizo chini ya Wizara hiyo.

Akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa majukumu katika kipindi cha Aprili hadi Juni, mwaka huu kwa kamati ya kusimamia ofisi za viongozi wakuu wa kitaifa ya baraza la wawakilishi iliyofanyika Ukumbi wa KVZ Mtoni Unguja.

Alisema tayari Wizara imeshawasilisha maeneo yanayohitaji kupatiwa hati miliki ya Wizara ya Ardhi nakulifanyia matengenezo jengo lake liliopo Vuga.

Waziri Masoud, aliutaja mkakati mwengine kuwa ni kuyafanyia matengenezo miundombinu ya umwagiliaji wa mazao ya kilimo kwa Jeshi la Kujenga Uchumi na Chuo cha Mafunzo ili viweze kuzalisha zaidi.

“Nitafuatilia masuala ya mrejesho wa fedha zinazokusanywa na serikali kuu kwenda Mamlaka za serikali za mitaa, ili kuziwezesha mamlaka za mitaa kutekeleza majukumu yake ipasavyo”, alisema.

Aidha, alifahamisha kuwa, wizara yake itaendele kununua vitendea kazi kupitia bajeti za ndani pamoja na kutafuta washirika wa maendeleo kusaidia upatikanaji wa magari ya usafi.