NA NASRA MANZI,WHVUM
KATIBU Mkuu Wizara ya Habari,Vijana,Utamaduni na Michezo Fatma Hamad Rajab, amesema Wizara itaendelea kushirikiana na wachezaji wa zamani wa mpira wa miguu ili kusudi kunyanyua michezo.
Akizungumza katika viwanja wa Mao Zedong Kikwajuni baada ya kuangalia mazoezi kwa Veterani wa Unguja ambao wanajiandaa na mchezo wa kirafiki unaotarajiwa kuchezwa Agosti 29 uwanja wa Gombani Pemba.
Alisema wazee wamekuwa na historia katika michezo mbali mbali,hivyo wizara itashirikiana nao katika kuhakikisha soka la Zanzibar linapiga hatua.
“Tutashirikiana na wazee wetu katika michezo ,kupokea ushauri, tunahitaji mpira upate mafanikio kwani wazee wetu walioanza michezo na sasa wanawaridhisha vijana” alisema
Aidha alimpongeza Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi kwa juhudi anazoendelea kuchukua katika kuimarisha michezo.
Alieleza kuwa michezo inaleta mashirikiano,upendo,na umoja,hivyo mchezo huo utaleta taswira ya kupata umoja.
Nae mchezaji wa zamani wa klabu ya KMKM Abdalla Maulid Abdalla alisema lengo la mchezo huo ni kufuata wito wa wizara katika kurejesha vuguvugu la michezo kwa wachezaji wa zamani.
Aliipongeza Wizara ya Habari,Vijana,Utamaduni na Michezo kwa kuendelea kuwathamini wachezaji wa zamani na kupokea ushauri wao ,sambamba na kuwa tayari kushirikiana na wizara ili kuona mpira unakua.
Mchezo huo unaotarajiwa kuwakutanisha Veterani wa Unguja na Pemba Agosti 29 katika Dimba la Gombani kisiwani Pemba.