NA ABDI SULEIMAN, PEMBA

TIMU ya Wizara ya Afya imefanikiwa kutwaa ubingwa wa mashindano ya Mawizara Pemba, baada ya kuibuka na ushindi wa mikwaju ya Penant 5-3 katika fainali ya mashindano hayo.

Hatua ya mikwaju ya Penant hiyo, ilikuja baada ya timu hizo kutoshana nguvu katika dakika zote za mchezo zikiwa zimefungana bao 1 – 1.

Kipindi cha kwanza kilianza kwa kasi kubwa uwanjani hapo, kila timu ikihitaji ushindi ili kuweza kuibuka bingwa wa mashindano hayo makubwa Kisiwani Pemba.

Licha ya Wizara ya Utalii na Mambo ya kale kuonekana kuwa imara kila idara, jitihada za walinzi na mlinda mlango wa Afya kuokoa michomo ya washambuliaji wa utalii ilipelekea timu hizo kwenda mapumziko bila ya kufungana.

Kipindi cha pili kilianza kwa kasi kubwa huku kila timu ikifanya mabadiliko ya wachezaji wao ambapo katika dakika ya 66 Afya ilipata bao la kuongoza kupitia kwa Mohamed Saleh Mohamed kabla ya Utalii kusawazisha bao hilo kupitia kwa Idrisa Abdalla Mohamed.

Fainali hiyo ilishuhudiwa na viongozi mbali mbali wa serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, wakiongozwa na Naibu Waziri wa mambo ya nje na ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mbarouk Nassor Mabarouk aliekuwa mgeni rasmi.

Katika fainali hiyo Mchezaji Mohamed Salum Mohad aliibuka mchezaji bora kutoka Afya, Ali Ussi kutoka Utalii aliweza kuibuka mfungaji bora, Omar Dadi Omar kutoka Utalii aliweza kuibuka kipa bora, huku mchezaji bora katika mashindano hayo kwa ujumla alikuwa ni Mussa Ali Mussa kutoka Timu ya ZECO.