TOKYO, JAPANI

WIZARA ya Afya ya Japani kwa mara ya kwanza imewataja hadharani watu waliovunja sheria zinazosimamia wasafiri wanaowasili nchini humo kutoka nje kujiweka kwenye karantini kwa kipindi cha siku 14.

Watu watatu wenye umri wa miaka kati ya 20 na 39 walitajwa kwenye tovuti ya wizara hiyo. Waliwasili nchini Japani Julai 21 kutoka Korea Kusini na Hawaii.

Watatu hao walipimwa na kutokutwa na virusi vya korona katika viwanja vya ndege walikowasili.

Wizara inamtaka kila mtu anayewasili nchini Japani kutoka nje kujitenga nyumbani au hoteli kwa siku 14.

Wanatakiwa kusaini fomu ya kuahidi kutumia programu ya simu aina ya smartphone kuripoti waliko na hali zao kila siku.

Wizara hiyo inasema watatu hao hawakutoa data za kuonyesha waliko kamwe na hawajapokea simu walizopigiwa kwa njia ya video, vitendo vyao vilichukuliwa kuwa vya kimakusudi.

Maofisa wanasema wanapanga kuendelea kuwataja hadharani watu wanaokiuka ahadi zao kutokana na kile wizara inachukulia kuwa dhamira mbaya.