NA JOSEPH DAVID

UONGOZI wa klabu ya Yanga umesema maandalizi ya uzinduzi wa wiki ya mwananchi, utafanyika Jumapili ya wiki hii visiwani Zanzibar.

Akizungumza na gazeti hili kwa njia ya simu afisa habari wa klabu hiyo Hassan Bumbuli, alisema tukio hilo litaonyeshwa moja kwa moja (Live), kwenye vyombo vya habari.

Alisema ratiba ya shughuli hiyo itaanza kwa kusoma dua kaburini kwa marehemu Mzee Abeid Karume ofisi ya CCM Kisiwandui, baadaye wataelekea hospitali ya Mnazimmoja kutoa msaada, ikiwa ni miongoni mwa matukio ambayo hufanyika kwenye wiki hiyo.

Bumbuli alisema baada ya kutoa msaada kwenye hospitali ya Mnazimmoja, mchana watafanya uzinduzi rasmi pale Kariakoo ukumbi ambao utatajwa baadae.

Baada ya uzinduzi huo wanachama, wapenzi na mashabiki wa klabu hiyo nchi nzima wataendelea kufanya shughuli mbalimbali za kijamii, ikiwemo kutoa misaada na kufanya usafi kwenye maeneo mbalimbali kwa wiki nzima, kulingana na walivyojipangia kwenye matawi yao.

Bumbuli alisema wamejipanga kuifanya wiki ya mwanachi ya msimu huu kuwa tofauti na misimu iliopita, kwani kutakuwa na mambo mbalimbali yatakayoleta utofauti mkubwa.

“Hatuwezi kusema tutafanya nini na nini, lakini tukisema maana yake tutakuwa tunaondoa ile hamu ya watu kujua nini kitafanyika, kwa hiyo muhimu ni kwamba wanayanga, wananchi washiriki kupitia matawi yao, lakini pia wale ambao wapo kwa mbali kwenye uzinduzi wasikilize kupitia vyombo vya habari” alisema.

Hii ni mara ya pili mfululizo kwa klabu ya hiyo kufanya uzindizi wa wiki ya mwananchi visiwani Zanzibar.

Kilele cha wiki ya mwananchi kitakuwa Agost 29 jijini Dar es Salaam huku siku hiyo kikosi chote kitakachotumika kwa msimu huu wakiwemo wachezaji wapya, waliosajiliwa na klabu hiyo watatambulishwa mbele ya halaiki ya mashabiki lukuki watakaokuwa wamefurika kwenye uwanja wa Benjamin Mkapa.