TRIPOLI, LIBYA

SHIRIKA la Wakimbizi la Umoja wa Matiafa (UNHCR) limesema kuwa, karibu wahamiaji 130 wameokolewa baharini na kurejeshwa nchini Libya.

Shirika hilo limetoa taarifa kupitia mtandao wa kijamii wa Twitter na kusisitiza kuwa, wahamiaji wapatao 130 wameokolewa kutoka katika boti mbili zilizopinduka na kuzama baharini.

Wahamiaji hao walirejeshwa Tripoli mji mkuu wa Libya.Taarifa hiyo ya UNHCR imeongeza kuwa, watu wanne hawajulikani walipo.Mara baada ya kuokolewa, wahamiaji hao walipewa huduma za kwanza za matibabu.

Wengi wa wahamiaji hao walikuwa na upungufu wa maji mwilini,uchofu wa kupindukia na kuungua.Siku chache zilizopita pia, Shirika la Wahamiaji Duniani (IOM) lilisema wahamiaji 17 wamekufa maji baada ya boti waliyokuwa wakisafiria kuzama katika pwani ya Libya.

Safa Msehli, msemaji wa shirika hilo la Umoja wa Mataifa alisema kuwa, boti hiyo iliyokuwa imebeba wahamiaji wapatao 70, ilizama nyakati za usiku katika mji wa Zuwara wa magharibi mwa Libya,ukiwa ni muendelezo wa matukio ya kufa maji wahamiajia wakiwa katika safari hatarishi za kujaribu kuelekea Ulaya.

Alisema, Gadi ya Pwani ya Libya imefanikiwa kuwaokoa wahamiaji 51 raia wa Misri katika tukio hilo, na kuopoa mwili mmoja katika Bahari ya Mediterania.

Watu wengine 16 hawakupatikana na inaamini walifariki dunia na kusombwa na maji.

Takwimu za Shirika la Wahamiaji Duniani (IOM) zinasema kuwa, tangu mwanzoni mwa mwaka huu wa 2021 hadi hivi sasa zaidi ya wahamiaji 22,000 wakiwemo wanawake na watoto wadogo wameokolewa katika fukwe za Libya huku mamia ya wengine wakipotea na inaaminika wamekufa maji.