KABUL, AFGHANISTAN
WATU wasiopungua 110 wameuawa na wengine kadhaa wamejeruhiwa kufuatia miripuko miwili ya mabomu iliyotokea nje ya uwanja wa ndege wa Kabul nchini Afghanistan.
Hospitali ya kituo cha upasuaji wa dharura mjini Kabul ilitangaza kuwa maiti 90 na makumi ya majeruhi wamefikishwa hospitalini hapo.
Taarifa ya awali iliyotolewa na Ofisa wa Taliban ilisema watu wasiopungua 13 walikuwa wameuawa katika miripuko hiyo.
Watoto wadogo ni miongoni mwa waliouawa katika miripuko hiyo ya mabomu iliyotokea kandokando ya uwanja wa ndege wa Kabul.
Hakuna mtu au kundi lolote lililotangaza kuhusika na hujuma hiyo ambayo ni ya kwanza kutokea mjini Kabul tangu rais Ashraf Ghani aitoroke nchi na mji mkuu huo wa Afghanistan kudhibitiwa na kundi la Taliban mnamo tarehe 15 Agosti.
Msemaji wa wizara ya ulinzi ya Marekani Pentago, John Kirby alisema, mripuko mmoja umetokea karibu na lango la Abbey la kuingilia uwanja wa ndege wa Kabul na mripuko wa pili umetokea jirani na hoteli ya Baron iliyopo karibu na uwanja huo.
Kwa mujibu wa Kirby, askari 13 wa Marekani ni miongoni mwa waliouawa katika mashambulio hayo.
Mwenyekiti wa Baraza Kuu la Maridhiano ya Kitaifa la Afghanistan Abdullah Abdullah alilaani hujuma hiyo akiitaja kuwa ni shambulio la kigaidi.
Maofisa wa Pentagon walisema, wanaitakidi kuwa kundi la kigaidi la ISIS ya Khorasan ndilo lililohusika na miripuko hiyo iliyotokea katika mazingira ya mtafaruku na msongamano wa watu waliomiminika katika uwanja wa ndege wa Kabul kwa lengo la kuihama nchi.