NA MWANDISHI WETU

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi amekutana na kufanya mazungumzo na Balozi wa Oman aliyemaliza muda wa uwakilishi nchini Tanzania,  Ali Bin Abdallah Bin Salim Al  Mahrooq.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari na Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Ikulu,  Abdul Van Mohamed, ilieleza kuwa viongozi hao walikutana jana ikulu mjini Zanzibar.

Taarif hiyo ilieleza kuwa katika mazungumzo hayo, Balozi Al Mahrooq alitumia fursa hiyo kumuaga rasmi Dk. Mwinyi huku akisisitiza kuendelezwa ushirikiano uliopo hususani katika sekta za kibiashara baina ya Oman na Zanzibar.

Aidha Balozi Al Mahrooq aliipongeza Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa kushirikiana na Oman wakati wa kipindi cha muda wake wa kuiwakilisha Oman  hapa nchini.

Balozi huyo alisema aliapa ushirikiano wa serikali ya Mapinduzi miradi ya  maendeleo mbalimbali ikiwemo uimarishwaji wa sekta ya elimu Zanzibar, kukarabati majengo ya Mji Mkongwe wa Zanzibar na miradi mingi ya maendeleo.

Kwa upande wake,  Dk. Mwinyi alimshukuru Balozi Al  Mahrooq kwa kazi nzuri aliyoifanya wakati wa uongozi wake na kuishukuru Oman kwa ushirikiano mkubwa na kumtaka afikishe salam kwa Sultan wa Oman, Haitham Bin Tariq Al Said.

Dk. Mwinyi alimueleza Balozi huyo kuwa Zanzibar iko tayari na itaendelea kushirikiana na Oman katika sekta mbalimbali za maendeleo ikiwemo kibiashara na kijamii hasa ikizingatiwa kuwa Oman na Zanzibar zina historia kubwa na ya kipekee.