NA NASRA MANZI, WHVUM
WAZIRI wa Habari,Vijana Utamaduni na Michezo Tabia Maulid amesema ujio wa viongozi wa mpira wa miguu kutoka Misri, umeahidi kuwekeza Zanzibar, katika michezo ili kuwapatia fursa na kunyanyua soka nchini.
Akizungumza na ugeni huo baada ya kuwasili ofisi za Wizara ya Habari,Vijana,Utamaduni na Michezo huko Migombani Mjini Unguja.
Alisema ujio huo utafungua milango na fursa za michezo kwa vijana pamoja na fursa nyengine za kuekeza katika utalii, kwa kisiwa cha Unguja na Pemba ili kuongezeka kwa wageni .
Tabia alieleza wameahidiana kurejesha utamaduni uliopo zamani kwa timu ya Taifa ya Zanzibar kwa kukaaa kambi nchini Misri kwa lengo la kupata uzoefu na mazoezi zaidi.
“ Viongozi wa mpira wa miguu kutoka Misri wametuahidi mambo mengi ya kutuletea maendeleo nchini kwetu, tumefarajika kama wizara, lakini pia serikali yetu ya awamu ya nane imetilia mkazo masuala ya michezo ,uwekezaji na kukuza utalii “ alisema
Alisema serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itaendelea kushirikiana na kudumisha mahusiano na serikali ya nchini Misri , kwa kutekeleza ilani na kumsaidia Rais wa Zanzibar Dk. Hussein Mwinyi katika kukuza mahusiano na nchi jirani.
Nae Mtendaji Mkuu (CEO) kutoka Kampuni ya Captex kutoka Misri Mohamed Hassan Abouzeid, alisema wapo tayari kuendelea kushirikiana na Zanzibar, katika kuimarisha na kukuza michezo ,pamoja na kuwekeza ili kuona mpira wa miguu Zanzibar unapiga hatua.
Aidha serikali ya Misri imeahidi pia kutoa vifaa vya michezo na uwekezaji na kuwekeza sehemu nyengine za utalii.
Nae Rais wa Chama Cha mpira wa miguu Zanzibar Abdulllatif Ali Yassin ametoa wito kwa wanamichezo nchini, husuan mpira wa miguu kuitumia fursa hiyo kwa wawekezaji hao kutoka nchini Misri , kwani wana lengo la kuwekeza katika soka la vijana sambamba na kuuza wachezaji nje ya nchi na pia kuimarisha viwanja na Academy