NA LAYLAT KHALFAN

KATIBU Mkuu wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Zanzibar (ZATUC), Khamis Mwinyi Mohammed, amewataka wajumbe wa kamati ya shirikisho hilo, kuendelea kusimamia jitihada mbali mbali za kutetea maslahi ya wafanyakazi katika maeneo yao ya kazi.

Katibu huyo, aliyasema hayo katika kikao cha Kamati Tendaji ya ZATUC, ambacho kilichojadili na kupitisha utendaji ya shirikisho hilo, kilichofanyika katika ukumbi wa Watu wenye Ulemavu Zanzibar.

Alisema hatua ya kuvisimamia vyama hivyo, itawajengea   wafanyakazi mazingira bora ya kazi na kuwahamasisha kutekeleza wajibu wao katika kufikia malengo yaliyokusudiwa.

Alisema wafanyakazi wana matumiaini mengi ambayo wanayahitaji kupitia ndani ya vyama hivyo, na ni vyema kamati hiyo ikiwa na moyo na ari ya kujadili yale yote yenye mnasaba na wafanyakazi, ili kupata maslahi bora huku wakitimiza wajibu wao kwenye kazi zao za kila siku.

Alifahamisha kuwa, kazi ya mwaajiri ni kutumia nguvu za mfanyakazi kwa maslahi yake hivyo ni vyema waajiriwa wakahakikisha wanatoa maslahi kutokana na kazi zao wanazozifanya.

“Mwajiri siku zote anataka nguvu za mtu kwa bei rahisi, hivyo waajiriwa mnatakiwa kuvitumia vyama hivi kwasababu vimewekwa kwa mujibu wa katiba na sheria za nchi”, alisema.

Alisema kikao hicho pia kina lengo la kujadili changamoto na mafanikio yanayojitokeza katika sekta ya ajira kwa mujibu wa sheria na taratibu zilizopo.

Akifungua kikao hicho, Mwenyekiti wa Shirikisho hilo, Ali Mwalimu Rashid, aliviomba vyama vya wafanyakazi na wafanyakazi kuviunga mkono, ili viweze kutetea maslahi yao kwa mujibu wa sheria.

“Faida na uhai ndani ya chama ni lazima kuwe na vikao maalum vitakavyojadili changamoto na mafanikio ya wafanyakazi kwa kuwa ndio tegemeo kubwa la wafanyakazi bila hivyo kutakuwa hakuna vyama,” alieleza Mwenyekiti huyo.

Baadhi ya wajumbe wa kamati hiyo, walisema kazi yao kubwa ni kuhakikisha wanapitia shughuli mbali mbali za vyama na kuandaa ajenda ya kikao cha baraza kuu kitakachofanyika hapo baadae.

Walisema vyama wafanyakazi mtaji wake ni wanachama, hivyo wakati umefika sasa kuchangamkia fursa hiyo, ili kufikia azma ya maslahi ya wafanyakazi kwa kuwatetea.

“Tunapojiunga pamoja tunapata nguvu nzuri ya kupeleka ushawishi katika utetezi wa mambo mbalimbali ikiwemo kulinda maslahi yetu”, alisema Katibu Mkuu wa Chama cha Wafanyakazi Mawasiliano, Uchukuzi na Usafirishaji, Amour Mussa Makame.